Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI KANDA YA KUSINI

HISTORIA FUPI YA KITUO

TALIRI Naliendele iko katika Mkoa wa Mtwara, Kusini mwa Tanzania, takriban kilomita 13 kusini mwa Manispaa ya Mtwara-Mikindani na kilomita 6 kusini-magharibi mwa Uwanja wa Ndege wa Mtwara. Kituo hiki kipo kwenye mwinuko wa mita 120 kutoka usawa wa bahari.

Kikiwa ni Kituo cha Kanda cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), TALIRI Naliendele kina jukumu la kusimamia tafiti za mifugo katika Kanda ya Kusini, inayojumuisha mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma. Kituo hiki kilianzishwa mwaka 1992 kama Programu ya Utafiti wa Mifugo, chini ya Mkurugenzi wa Utafiti wa Kilimo na Maendeleo – Naliendele.

Mwaka 1995, programu hii ilibadilishwa rasmi na kuwa Kituo cha Utafiti wa Mifugo. Baadaye, mwaka 2012, kituo hiki kilipokea jina rasmi la TALIRI Naliendele, kwa mujibu wa Sheria Na. 4 ya mwaka 2012 iliyoanzisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI).Mbali na kituo kikuu cha Naliendele, TALIRI pia inasimamia Kituo cha Utafiti cha Mnima, kilichopo Wilaya ya Newala.

 

MAJUKUMU YA JUMLA YA KITUO CHA TALIRI NALIENDELE

Majukumu ya ya Kituo cha TALIRI Naliendele ni kufanya tafiti za mifugo na malisho katika Kanda ya Kusini kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa mifugo. Kulingana na muundo wa TALIRI wa tarehe 7 Novemba 2013 (TALIRI – Organizational Structure Document), TALIRI – Naliendele imepewa mamlaka ya kuwa kituo kikuu cha utafiti wa kuku na jamii nyingine za ndege wanaofugwa (Poultry) ndani ya nchi. Kwa ujumla kituo kina majukumu yafuatayo:

 

  1. Kuibua teknolojia sahihi, kuzifanyia majaribio na tathmini na kutunza rasilimali za mifugo yenye sifa za kipekee kama ustahamilivu wa magonjwa na ukame, na uwezo wa kuzaa mapacha nk;
  2. Kutoa utaalam juu ya maudhui yanayohusiana na uzalishaji, vyakula vya mifugo na ulishaji, malisho, matunzo ya mifugo, utunzaji wa mazingira na utafiti wa mifugo;
  3. Kushirikiana na maabara za kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kuthibitisha, kufanya majaribio na kuweka viwango vya utafiti na uzalishaji wa mifugo.
  4. Kuibua teknolojia kwa ajili ya kufanya tathimini vituoni na mashambani ya koosafu za mifugo ya asili na kisasa.
  5. Kusimamia na kuwafundisha wanafunzi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kitaifa na kimataifa.
  6. Kuimarisha mahusiano kati ya watafiti, maafisa ughani, wafugaji na wadau wengine katika Kanda ili matokeo ya tafiti za mifugo ziwafikie walengwa.