Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
Masuala ya Kijamii na Kiuchumi

Taasisi inatekeleza miradi mbalimbali ya utafiti  wa mifugo kwa kuzingatia masuala muhimu ya jinsia, mazingira na ustawi wa jamii kiuchumi. Ni imani yetu kuwa ili ufugaji uwe endelevu lazima uzingatie masuala muhimu mtambuka ambayo pia yanasisitizwa na kujumuishwa kwenye agenda za kitaifa na kimataifa. Taasisi imekuwa mstari wa mbele katika kubuni miradi inayoweza kusaidia makundi maalumu hasa wanawake na vijana ambao kwa asili ya tamaduni zetu hawapati nafasi ya kumiliki njia kuu za uzalishaji mali. Miradi kama ya kopa ng'ombe lipa ngómbe, miradi ya kusambaza kuku chotara (Sasso, Kuroiler, Tanbro,) kwa akina mama na wafugaji wengine wadogo wadogo ni mfano halisi namna inavyolenga kuwanufaisha wadau waliopo katika makundi maalumu na pia kuleta ustawi wa kiuchumi na kijamii. Taasisi imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali inayolenga kupanda miti malisho na majani maeneo ya kuchungia, kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira, kupunguza ufugaji wa kuhamahama na kuzalisha malisho ya kutosha. Pia imekuwa ikisaidia kuelimisha wafugaji namna ya kufuga kulingana na uwezo wa eneo ulionalo bila kuathiri mazingira. Na hivi karibuni tumeanza kufanya utafiti wa kuchunguza kiasi cha hewa ukaa inayozalishwa kutokana na shughuli za ufugaji na namna ya kupunguza kwa kuchagua  mbari bora huku ukilisha malisho na lishe bora.

Taasisi imekuwa ikitekeleza miradi mahsusi inayolenga masuala ya kiuchumi, kijamii, mazingira endelevu, tekinolojia na ustawi wa jamii. Miradi hiyo inalenga maeneo yafuatayo:

1. Kukuza uchumi wa wafugaji na wadau wote katika mnyololo wa thamani kwa kkuwapa tekinolojia za kisasa zenye tija zaidi

2. Miradi inayolenga kuwafanya wafugaji wafuge kibiashara kwa kupata mbari bora na malisho 

3. Kufanya miradi inayolenga kuhifadhi mazingira na kuufanya ufugaji uwe endelevu

4. Miradi inayolenga kuwainua wanawake na vijana kuwa wafugaji wa kibiashara na wafanyabiashara katika mnyololo wa sekta ya mifugo

5. Miradi inayolenga kuwainua wabunifu wa tekinolojia na vijana wajasiriamali wenye nia ya kufanya mapinduzi katika sekta ya mifugo kwa kupitia tekinolojia za kisasa kwa kukifanya kilimo kuwa rahisi zaidi

6. Kutoa elimu za biashara, fedha, ujasiriamali, jinsia na mazingira

7. Miradi inayolenga kuinua kiuchumi jamii za watu wanaoishi kwenye umaskini na hawana uhakika wa kipato na chakula cha kila siku