Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI NA ZALIRI KUSHIRIKIANA KUTUNZA MBARI ZA MIFUGO YA ASILI
13 Aug, 2025
TALIRI NA ZALIRI KUSHIRIKIANA KUTUNZA MBARI ZA MIFUGO YA ASILI

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Zanzibar (ZALIRI) Dkt. Abdallah Ali amesema ZALIRI itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) katika kuhakikisha mbari bora za mifugo ya asili ya kitanzania zinaendelea kuboreshwa na kutunzwa kwa maslahi ya wafugaji.

Hayo ameyaeleza leo tarehe 05/08/2025 alipotembelea banda la TALIRI lililopo ndani ya viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma yanapoendelea Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ‘Nanenane’ na kujionea Teknolojia bora za mifugo zilizozalishwa na taasisi hiyo ikiwemo ya malisho na mbegu za malisho, mbari bora za mifugo na vyakula vya mifugo.

Dkt. Abdallah ameendelea kueleza mbali na taasisi hizo kuendelea na tafiti za kuchanganya mbari za mifugo ya asili na mifugo ya kigeni bado inajukumu la kuendelea kutunza mbari za mifugo ya ya asili ya kitanzania kwani na yenyewe inasifa za kipekee ikiwemo ustahimilivu wa magonjwa na ukame.

Sambamba na hayo Dkt. Abdalllah amesema amefurahishwa na mradi wa kuboresha kuku wa asili aina ya Horas unaotekelezwa na TALIRI kwani utaongeza tija kwenye ufugaji wa kuku wa asili.

Akiongelea mradi huo Meneja wa Sehemu ya Uhaulishaji wa Teknolojia Bw. Gilbert Msuta ameeleza kuwa Mradi huo unatekelezwa kwa lengo la kupata kuku wa asili mwenye uwezo wa kutaga mayai 200 - 240 kwa mwaka na kufikia uzito wa kilo 1.5 ndani ya wiki 16.

Msuta amendelea kueleza kuwa kuku hao ni bora kwenye uzalishaji kwani kuku wengine wa asili wasioboreshwa hufikia uzito wa gramu 1,200 - 1,500 kwa mwaka na kutaga wastani wa mayai kati ya 30 - 45 kwa mwaka.