Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI KANDA YA KATI

Kihistoria, shughuli za utafiti wa mifugo hapa nchini zimekuwa zikiratibiwa toka Mpwapwa. Kwa takribani kwa miongo nane (8), Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Kituo cha Mpwapwa (TALIRI Mpwapwa), ikitambulika kwa majina tofauti kwa nyakati tofati, kimekuwa ni kitovu cha shughuli za utafiti wa mifugo hapa nchini Tanzania. Kituo hiki kilianzishwa na Serikali ya Ujerumani mwanzoni mwa karne ya ishirini (mnamo mwaka 1905), na kilitumika kama Kituo cha utafiti wa magonjwa ya wanyama hadi wakati wa vita kuu ya kwanza ya Dunia. Kwa bahati mbaya, hakukuwa na vielelezo vya kutosha vilivyoachwa, vya kazi zilizofanyika, isipokuwa uwepo wa josho la kuogeshea mifugo lililoanzishwa mwaka 1905. Josho hili inaaminika ni josho la kwanza kujengwa na kutumika katika nchi za ukanda wa Afrika ya mashariki, na linaendelea kutumika kuogeshea mifugo hadi sasa.

Mwaka 1922, Kituo kilichukuliwa na Serikali ya Uingereza, ambayo ilianzisha maabara ya uchunguzi wa magonjwa ya wanyama. Mwaka 1924 hadi 1929 kazi kuu za kituo zilikuwa ni utafiti wa magonjwa ya sotoka na ndorobo. Dozi zaidi ya 50,000 za chanjo ya ugonjwa wa sotoka zilizalishwa kila mwaka katika kituo hicho. Mwaka 1929 Makao Makuu ya Idara ya Tiba na Utunzaji wa Wanyama yalihamishiwa Dar es salaam. Aidha, inaelezwa kuwa mnamo mwaka 1923 kazi ya za uboreshaji mbari za mifugo ilianzishwa, kwa ng’ombe wa asili wa hapa nchini, wanaopatikana katika mikoa ya Iringa, Rungwe, Singida, na kutoka katika jamii za wamaasai, kupitia mpango wa upandishaji (crossbreeding).

Kuanzia mwaka 1930 hadi 1938 shughuli za utafiti na utunzaji wa mifugo zilipata hadhi ya juu kwa kuteuliwa mtaalamu wa bayokemia (Biochemist) na Afisa Utafiti katika nyanja za malisho. Majaribio kadhaa ya kitafiti katika nyanja ya lishe ya wanyama na matunzo ya malisho yaliyafanyika hapa kituoni na katika mazingira ya wafugaji na kuripotiwa katika ripoti za mwaka na katika jarida la kilimo la Afrika ya Mashariki. Shughuli za uzalishaji wa wanyama zilizidi kupanuliwa kwa kuteuliwa kwa mtaalam wa vinasaba (Geneticist) mwaka 1944. Mnamo mwaka 1951 ofisi ya usajili wa mifugo ilianzishwa.  Pia katika kipindi hicho, kituo kilifanya juhudi zaidi ya kuendeleza sekta ya mifugo ambapo Kituo cha Mafunzo ya Tiba na Utunzaji wa Wanyama kilianzishwa.

Mnamo mwaka 1954, Makao Makuu ya Divisheni ya Tiba na Utunzaji wa Wanyama yalirudishwa Dar es salaam, ambapo Daktari Mkuu wa Mifugo alibakia Mpwapwa akiratibu shughuli za maabara ya utafiti, Kituo cha uzalishaji mifugo na shughuli za utafiti wa mifugo na malisho. Katika miaka hii ya mwanzoni mwa karne ya 20, kituo kilijipatia sifa kimataifa katika shughuli za kitafiti zinazohusisha uzalishaji wa wanyama, lishe ya wanyama, na utunzaji na matumizi bora ya malisho. Wanyama waliokuwa wakizalishwa na kutunzwa kituoni wakati huo ni ng’ombe, nyati maji, kondoo, mbuzi, nguruwe, kuku na farasi.

Mwaka 1962, yalifanyika mabadiliko ya kimuundo ambayo yaliziweka pamoja, chini ya Divisheni ya Utafiti, Taasisi zote zilizokuwa zikishughulika na majaribio na utafiti katika Nyanja za mazao na mazingira, utunzaji wa mifugo na uvuvi. Hivyo, kituo hiki kilibadilishwa na kuwa Kituo cha Majaribio ya Mifugo. Mwaka 1966 sera ya maendeleo ya mifugo ilihimiza usambazaji wa ng’ombe bora katika vijiji, na hivyo Kituo kilijikita zaidi katika uzalishaji wa ng’ombe hapa kituoni. Kituo kilibadilishwa tena na kuwa Kituo cha Uzalishaji wa Mifugo. Mwishoni mwa miaka ya 1960 kituo kilibadilishwa jina na kuwa Taasisi ya Utafiti na Mafunzo na ilijikita zaidi katika maendeleo ya sekta ya mifugo.

Kuanzia mwaka 1977 shughuli za utafiti na mafunzo zilitenganishwa na kuwa Taasisi zinazojitegemea ambapo shughuli za utafiti zilisimamiwa na Mkurugenzi na zile za mafunzo zilisimamiwa na Mkuu wa Chuo. Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ilikuwa ikitambulika kama Taasisi ya Utafiti na Uzalishaji wa Mifugo (LPRI), na jina hilo hilo liliendelea kutumika lilipoanzishwa Shirika la Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRO) Julai, 1981. Mnamo mwaka 1989 Shirika la Utafiti wa Mifugo Tanzania lilivunjwa na Taasisi kurejeshwa kuwa Taasisi ya Utafiti na Uzalishaji wa Mifugo, hadi mwaka 1999. Katika kipindi hicho, kanda za utafiti wa mifugo na mazao zilianzishwa kutokana na sifa ya ikolojia ya eneo husika, ambapo kituo cha kanda ya kati kilikuwa kikihudumia mikoa ya Dodoma na Singida. Kanda hiyo ilikuwa na jumla ya vituo  vinne (4) vya utafiti; viwili vya utafiti wa mazao (Makutupora na Hombolo) na viwili vya utafiti wa mifugo (LPRI – Mpwapwa na Kituo cha Utafiti wa Malisho – Kongwa). Makao Makuu ya Kanda yalikuwa ni LPRI – Mpwapwa. Hivyo, Mkurugenzi wa LPRI – Mpwapwa alikuwa pia ndiye Mkurugenzi wa Kanda.

Mwaka 2000 hadi 2005 shughuli za utafiti wa mifugo zilihamishiwa katika Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo chini ya Kurugenzi ya Utafiti na Mafunzo. Kuanzia mwaka 2006 hadi 2007 kazi za utafiti wa mifugo zilikuwa zikiratibiwa na Kurugenzi ya Utafiti, Mafunzo na Ugani chini ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo. Mwaka 2008 hadi 2012 shughuli za utafiti wa mifugo zilikuwa zikiratibiwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Mifugo – Mpwapwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Kutokana mahitaji ya fedha za utafiti na uboreshaji wa huduma za utafiti nchini, Sera ya Taifa ya Mifugo ya Mwaka 2006 iliona umuhimu wa uwepo wa Taasisi huru itakayoratibu shughuli za utafiti wa mifugo hapa nchini. Hii ilipelekea kuanzishwa kwa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), kwa sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, namba 4 ya mwaka 2012, kama ilivyotangazwa katika Gazeti la serikali namba 30 juzuu 93 la tarehe 27 Julai, 2012. Mwanzoni, Makao Makuu ya TALIRI yalikuwa Mpwapwa kabla ya kuhamishiwa Dodoma mwaka 2017. TALIRI ina na jumla ya vituo nane (8) vya utafiti vilivyo katika kanda saba (7) zenye ikolojia tofauti. Vituo hivyo ni; Mpwapwa and Kongwa (Kanda ya kati), Mabuki (Kanda ya ziwa), Naliendele (Kanda ya kusini), Tanga (Kanda ya mashariki), Uyole (Kanda ya nyanda za juu kusini), Nsimbo (Kanda ya magharibi) na West Kilimanjaro (Kanda ya kaskazini).

SHUGHULI ZINAZOFANYWA NA TALIRI MPWAPWA

  1. Utafiti unaolenga kuongeza kasi ya uzalishaji wa mifugo bora na mazao yake hapa nchini kwa kutumia teknolojia ya uhawilishaji viinitete (Embryo Transfer). Utafiti huu umehusisha upandikizaji wa viinitete katika jumla ng’ombe majike 18. Kazi hii imefanyika kwa ushirikiano kati ya TALIRI, Chuo Kikuu cha Illinois, na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
  2. Uhifadhi na uzalishaji wa ng’ombe aina ya Mpwapwa ukilenga kuhifadhi koosafu, na kuongeza uwezo wa kituo kusambaza teknolojia hii kwa wafugaji.
  3. Utafiti unaolenga kuzalisha ng’ombe bora wa maziwa anayeweza kuzalisha lita 10 hadi 16 kwa siku, na kustahimili mazingira ya mfugaji.
  4. Utafiti unaolenga kuzalisha, kuhifadhi na kusambaza mbegu na malisho bora ya mifugo kwa wafugaji ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mifugo nchini. Aidha, taasisi kwa kushirikiana na Taasisi ya serikali ya urasimishaji wa mbegu za nafaka na mazao mbalimbali (Tanzania Official Seed Certification Institute (TOSCI)) imetoa ithibati ya mbegu aina tatu za mikunde na aina mbili za nyasi na hivyo kutoa kibali cha kuzalishwa kwa wingi. Mbegu zilizopatiwa ithibati ni aina tatu za mikunde (Medicago sativa, Desmodium intortum na Macroptilium atropurperium) na aina mbili za nyasi (Cenchrus ciliaris na Chloris gayana).
  5. Mradi wa Utafiti wa African Dairy Genetic Gain (ADGG) unaolenga kuongeza tija ya uzalishaji wa maziwa kwa wafugaji wadogo wadogo hadi wakubwa katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Iringa na Mbeya. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya TALIRI Mpwapwa, Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa mifugo (ILRI), Chuo kikuu cha New England-Australia na Chuo Kikuu cha Scotland (SRUC).
  6. Tafiti na uhifadhi, uzalishaji, uboreshaji na usambazaji wa mbuzi bora kwa kutumia aina mbalimbali za mbuzi wa asili hapa nchini, mfano, Gogo white, Newala, na Ujiji (Buha).
  7. Utafiti unaolenga kuzalisha, kuhifadhi na kusambaza mbuzi bora aina ya Malya (Blended goats).
  8. Pamoja na shughuli za utafiti, Kituo kinashirikiana na Halmashauri za kanda ya kati (Dodoma na Singida) katika kutoa elimu (outreach programmes) juu ya teknolojia mbalimbali za malisho na mbegu za malisho, ufugaji bora wa kuku, ng’ombe, nguruwe, na mbuzi.

 

ORODHA YA VIONGOZI WALIOINGOZA TALIRI MPWAPWA

  1.  1905 – 1921
  2.  1922 – 1929 H. Honby
  3.  1930 – 1945 H. J. Howe
  4.  1945 – 1953 N. R. Reid
  5.  1954 – 1956 A. H. Mine
  6.  1957 – 1964 H. G. Hutchison
  7.  1965 – 1968 M. L. Kyomo
  8.  1969 – 1971 L. L. Ilmolelian
  9.  1971 – 1972 R. A. Chiomba
  10.  1972 – 1973 F. L. B. Mwijage
  11.  1973 – 1977 A. M. Macha
  12.  1977 – 1978 P. M. J. Katyega
  13.  1978 – 1981 D. B. Mpiri
  14.  1981 – 1982 P. M. J. Katyega
  15.  1982 – 1985 M. L. Kusekwa
  16.  1986 – 1988 D. B. Mpiri
  17.  1989 – 1992 S. M. Das
  18.  1993 – 1997 J. K. K Msechu
  19.  1998 – 2002 D. S. C. Sendalo
  20.  2002 – 2003 S. M. Das
  21.  2003 – 2007 J. N. M. Bwire
  22.  2007 – 2008 R. P. Mbwile
  23.  2009 – 2012 D. S. C. Sendalo
  24.  2013 – 2015 D. M. Komwihangilo
  25.  2015 – 2020 E. C. Kimbi
  26.  2020 – 2021 A. R. Chawala
  27.  2022 –           M. L. Kabululu