FENSI YA UMEME NI SULUHISHO LA KUONGEZA TIJA KWA WAFUGAJI, DKT NZIKU
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku amesisitiza umuhimu wa kufunga fensi ya umeme kwenye mashamba makubwa ya malisho ili kulinda rasilimali za mifugo na kuongeza tija katika uzalishaji.
Dkt. Nziku ametoa msisitizo huo tarehe 19/02/2016 kwa wafugaji wa Muheza, mkoani Tanga, wanaonufaika na Mradi wa Maziwa Faida, walipotembelea shamba la ‘Ndoto Farm’ mkoani Iringa kwa lengo la kujifunza mbinu bora za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na usimamizi wa malisho.
Akielezea kuhusu teknolojia hiyo, amesema kuwa fensi ya umeme husaidia kudhibiti mifugo isivuke mipaka ya eneo lililotengwa pamoja na kuzuia wanyama waharibifu kuingia kwenye mashamba ya malisho. Alifafanua kuwa hatua hiyo inahakikisha upatikanaji wa malisho bora kwa wakati wote, hupunguza hasara zisizo za lazima na husaidia kuimarisha mahusiano kati ya wafugaji na wakulima kwa kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi.
Aidha, Dkt. Nziku alieleza kuwa matumizi ya fensi ya umeme ni njia ya kisasa na yenye gharama nafuu kwa muda mrefu, kwani inapunguza upotevu wa mifugo, gharama za ulinzi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shamba.
Aliongeza kuwa TALIRI itaendelea kutoa mafunzo na ushauri wa kitaalamu kwa wafugaji ili kuwahamasisha kutumia teknolojia mbalimbali zitakazochochea maendeleo endelevu ya sekta ya mifugo nchini.
Kwa upande wake, Bw. Edward Chambaye mmoja wa wafugaji walioshiriki ziara hiyo alishukuru kwa mafunzo waliyoyapata, akisema yamewafungua macho kuhusu umuhimu wa teknolojia katika kuboresha uzalishaji wa maziwa.
Alieleza kuwa maarifa waliyopata kuhusu matumizi ya fensi ya umeme na usimamizi bora wa malisho yatawasaidia kuongeza uzalishaji, kupunguza hasara na kuboresha kipato chao pamoja na kuinua ustawi wa familia zao.
Ziara hiyo ni kwa hisani ya Mradi wa Maziwa Faida unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland Tanzania na kutekekezwa TALIRI kwa kushirikiana na Taasisi ya Mamlaka ya Chakula Ireland (Teagasc) ukilenga kuboresha mnyororo wa thamani wa ng’ombe wa maziwa.
