KATIBU TAWALA MKOA WA TANGA AIPONGEZA TALIRI KWA KUENDELEA KUSAMBAZA TEKNOLOJIA ZA MIFUGO
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Bw. Rashid Mchatta ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa juhudi zake za kuendelea kusambaza teknolojia na kutoa elimu kwa wananchi na wadau wa sekta ya mifugo, akisema hatua hiyo ina mchango mkubwa katika kuimarisha ufugaji wa kisasa na wenye tija nchini. Bw. Mchatta ametoa pongezi hizo leo July 09, 2026 alipotembelea banda la TALIRI katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam. Amesema TALIRI imeendelea kutekeleza kwa ufanisi jukumu lake la kufanya tafiti na kuhakikisha matokeo ya tafiti hizo yanawafikia wafugaji kupitia utoaji wa elimu, ushauri wa kitaalamu na usambazaji wa teknolojia mbalimbali zinazosaidia kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya mifugo. Akitoa maelezo kuhusu teknolojia zinazotolewa na taasisi hiyo, Mtafiti wa TALIRI, Bw. John Diyu, amesema taasisi inaendelea kuwahamasisha wafugaji, wawekezaji na wadau wote wa sekta ya mifugo kutembelea banda la TALIRI ili kupata elimu na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa watafiti. Bw. Diyu amebainisha kuwa katika banda hilo, wananchi wanapata elimu kuhusu malisho na mbegu bora za malisho zilizosajiliwa, mbari bora za mifugo pamoja na teknolojia nyingine mbalimbali zilizobuniwa na TALIRI kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa mifugo. “Kupitia elimu hii, wafugaji wanajifunza namna sahihi ya kuanzisha na kusimamia mashamba ya malisho, kuhifadhi malisho na kuandaa lishe bora kwa mifugo. Hii husaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama pamoja na kuboresha afya ya mifugo,” amesema Bw. Diyu. TALIRI inaendelea kuwakaribisha wananchi na wadau wote wa sekta ya mifugo kutembelea banda lake katika Maonesho ya Sabasaba ili kujionea teknolojia mbalimbali zinazotokana na tafiti, kupata ushauri wa kitaalamu na kujifunza mbinu bora za ufugaji wa kisasa wenye tija.
