WANANCHI WAENDELEA KUNUFAIKA NA ELIMU YA MALISHO KATIKA BANDA LA TALIRI
Wananchi na wadau mbalimbali wanaoendelea kutembelea banda la Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), wanaendelea kunufaika na elimu kuhusu kilimo cha malisho, matumizi ya mbegu bora za malisho pamoja na mbinu bora za uandaaji wa chakula cha mifugo inayotolewa na wataalamu wa taasisi hiyo. Elimu hiyo inatolewa katika banda la TALIRI lililopo katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo za kusambaza teknolojia na maarifa yatakayowasaidia wafugaji kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya mifugo. Kupitia maonesho hayo, wananchi na wadau wamepata fursa ya kujifunza namna ya kuzalisha malisho bora, kuchagua mbegu zenye ubora kulingana na mazingira yao, pamoja na kuandaa chakula cha mifugo chenye uwiano sahihi wa virutubisho muhimu ikiwemo protini, wanga, madini na vitamini vinavyohitajika kwa ukuaji, afya na uzalishaji wa mifugo. Aidha, wataalamu wa TALIRI wamewahimiza wafugaji kuwekeza katika uzalishaji wa malisho bora na matumizi ya teknolojia za kisasa za uhifadhi wa chakula cha mifugo ili kuhakikisha upatikanaji wa lishe bora kwa mifugo katika misimu yote ya mwaka, hatua itakayochangia kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na kuboresha kipato cha wafugaj
