Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI

Shughuli za Utafiti wa Mifugo katika kanda ya Nyanda za Juu Kusini zilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1970 lilipoanzishwa Shirika la Kilimo Uyole (SKU) kwa ufadhili wa nchi za Scandinavia (Norway, Denmark, Sweden, Finland na Iceland), kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Shughuli za utafiti ziliendelea hadi mwaka 1993 shirika lilipovunjwa. Baada ya SKU kuvunjwa, shughuli za utafiti wa mifugo ziliendelea chini ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika (1993 hadi 1995), Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo (1995 hadi 2012) na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (1995 hadi 2012). Kuanzia mwaka 2012 shughuli za utafiti wa Mifugo zilihamishiwa katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) ambayo ilianzishwa kwa sheria Na. 4 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2012.

Shughuli za Utafiti wa Mifugo katika kanda ya Nyanda za juu Kusini zinaendeshwa na Kituo cha Utafiti wa Mifugo Uyole ambacho kinahudumia Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa. Utafiti umeelekezwa kwenye kutathmini aina za mifugo, vyakula, malisho na huduma kwa mifugo ambazo zinaleta uzalishaji bora na wenye tija katika kanda hii.  Mkazo mkubwa umewekwa katika kuzalisha ng’ombe wa maziwa na chotara kwa ajili ya maziwa, pia nguruwe, kuku na malisho kwa ajili ya mifugo. Miaka ya hivi karibuni kituo kimekuwa mahiri sana kwa uzalishaji wa malisho jamii ya Rhodes na Napier.

MIRADI YA UTAFITI

Taasisi inafanya tafiti mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa  Mifugo, zipo tafiti zinazofanyika kituoni (on-station research) na zinazofanyika kwa wafugaji au wadau wa mifugo (on-farm research). Tafiti zote zinafanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo toka ndani na nje ya nchi.

Tafiti zinazofanyika Kituoni (On-Station Research)

  1. Mradi wa kuzalisha ng’ombe bora wa maziwa aina ya Friesian

Lengo la mradi huu ni kutunza na kuzalisha kinasaba cha ng’ombe bora wa maziwa aina ya Friesian. Vile vile mradi huu unalenga kusambaza ng’ombe bora wa maziwa aina ya Friesian kwa wafugaji waliopo ndani na nje ya Kanda hii.

  1. Mradi wa kuzalisha ng’ombe chotara wa maziwa

Lengo la mradi huu ni kuzalisha ng’ombe chotara wa maziwa wenye damu ya Friesian kwa asilimia 75% na damu aina ya Fipa kwa asilimia 25% na kuwasambaza kwa wafugaji mbali mbali katika Kanda.

  1. Mradi wa Kutafiti na kuzalisha malisho bora ya mifugo

Lengo la mradi huu ni kutafiti na kusambaza mbegu za malisho bora kwa wafugaji nchini. Aina ya malisho yanayozalishwa kituoni ni Rhodes (Chloris gayana), Napier (Pennisetum spp), miti malisho kama vile Lucina, Sesbania na Gliricidia, pamoja na malisho jamii ya mikunde kama vile alfalfa n.k. Kituo kimekuwa kikizalisha mbegu za malisho na kusambaza kwa wafugaji mbalimbali nchini.

  1. Mradi wa kurasimisha (certify) mbegu bora za malisho

Takwimu za awali za mofoloji kama Uotaji wa  mbegu, ukuaji, kuhimili wadudu, nk  kwa aina  nane (8) za malisho bora ya mifugo  zimekusanywa.  Malisho hayo ni Medicago sativa (Alfa alfa 6984), Desmodium intortum (Green leaf 104), Neonotonia wightii (ILRI 6761), Desmodium uncinatum (Silver leaf 6765). Macroptilium atropurureum (Siatro 12391), Chloris gayana (Rhodes grass 6633), Cenchrus ciliaris na Chloris gayana (Boma) – Uyole.

  1. Tathmini ya matumizi ya kimea cha pombe kama chakula mbadala cha nguruwe wanaokua

Lengo la mradi huu ni;

  • Kutathmini aina na viwango vya viinilishe vilivyomo kwenye kimea cha pombe.
  • Kutathmini kiwango sahihi cha kimea cha pombe katika utengenezaji wa chakula cha nguruwe wanaokua.
  • Kuhamasisha matumizi ya kimea cha pombe kama chakula cha nguruwe wanaokua.
  • Matokeo ya awali ya kituoni (on-station) yanaonyesha kwamba kimea cha pombe kinaweza kutumika kama chanzo cha protini kwa kulishia nguruwe. Kwa sasa Taasisi inalenga kutafiti matokeo yaliyopatikana kituoni kwenda kwenye mazingira ya wafugaji (on-farm).
  1. Kutathmini uzalishaji na uhimilifu wa aina mbali mbali za malisho aina ya Brachiaria zilichoguliwa miongoni mwa zinazopatikana Tanzania Bara

Lengo kuu la mradi huu ni kutambua aina gani ya malisho hayo inafanya vizuri kwenye mazingira gani na kanda ipi. Kwa sasa majaribio yanaenda sambamba kwenye kanda nne ambazo ni Kanda ya Ziwa (TALIRI-Mabuki), Kanda ya Kati (TALIRI-Mpwapwa), Kanda ya Mashaririki (TALIRI –Tanga) na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (TALIRI-Uyole).

Aina za malisho ya Brachiaria yanayoendelea kufanyiwa majaribio kwa kanda tajwa ni Geita 67, Kagera E85, Shinyanga E60, Geita E71, Geita E74, Kilimanjaro, S4E1, Arusha S3E1, Mtwara S2E3, Dodoma S1E1, Basilisk na Piata.

Tafiti zinazofanyika kwa wafugaji (On-Farm Research)

Hii ni miradi ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea upatikanaji wa fedha kutegemeana na maandiko (Research proposals) na pia ushirikiano na wadau mbalimbali kwenye eneo la uendelezaji teknolojia za mifugo.  Katika kipindi cha mwaka 2015/16 hadi 2021/22 jumla ya miradi mitatu imetekelezwa katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

  1. African Chicken Genetic Gains Program (ACGG)

Mpango huu ulilenga kupata, kupima, kurekebisha na kuchochea mahusiano ya serikali na sekta binafsi kwa kuzidisha na kuongeza upatikanaji wa pembejeo za bei nafuu ili kukuza uzalishaji wa kuku kwenye nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. Aidha, nchi tatu  (Tanzania, Ethiopia na Nigeria) ziliingizwa kwenye mradi huu kati ya mwaka 2015 hadi 2020 na ulipata pesa kutoka Bill & Melinda Gates Foundation (B&MGF). Kwa kanda hii jumla ya vijiji 16 vya Halmashauri za wilaya ya Mbeya, Ileje, Wanging’ombe na Njombe zilishirikishwa. Katika vijiji hivyo jumla ya  wafugaji 320 walishiriki katika mradi na kupatiwa kuku 25 kila mmoja, hivyo kuleta jumla ya kuku 8000 kwa wafugaji wote.

  1. African Dairy Genetic Gains Program (ADGG)

Mpango huu unatekelezwa Ethiopia na Tanzania na unafadhiliwa na Bill & Melinda Gates Foundation (B&MGF). Mpango unalenga kuboresha mbari/kosaafu za ng’ombe wa maziwa kwa kuboresha mfumo wa ukusanyaji na matumizi ya kumbukumbu za uzalishaji kwa kutumia TEHAMA. Kwa kuanzia mradi unafanyika kwenye mikoa inayozalisha maziwa kwa wingi (Milk shed areas) yaani Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya/Songwe na Iringa/Njombe.

  1. Climate Smart Dairy

Mradi huu unatekelezwa katika nchi ya Tanzania na Rwanda na unapata ufadhili kutoka  IFAD. Kwa Tanzania mradi unaratibiwa na TALIRI Tanga na Mabuki na kwa kuanzia unatekelezwa katika wilaya za Mufindi, Njombe na Rungwe. Lengo kuu la mradi ni kuongeza uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa kwa kutumia malisho yaliyoboreshwa aina ya Cayman, Lablab, Desmodium, Stylosanthes, Cobra, Chloris gayana na Guatemala ambayo yanazingatia kutoathiri mabadiliko ya tabia nchi na utoaji wa gesi ukaa (GHGs).

VIONGOZI WALIOONGOZA

Wafuatao ni viongozi walioongoza TALIRI Uyole katika vipindi tofauti tofauti

  1. Dr. Edwin Peter Chang’a – 2019 hadi sasa.
  2. Dr. Selemani Masola – 2017 hadi 2019
  3. Dr. Pilika Mwakilembe – 2008 hadi 2017
  4. Dr. Mbwile – 1993 hadi 2007.