Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
WAFUGAJI WATAKIWA KUHAKIKISHA WANA MALISHO YA MWAKA MZIMA KABLA YA KUANZA KUFUGA
20 Feb, 2026
WAFUGAJI WATAKIWA KUHAKIKISHA WANA MALISHO YA MWAKA MZIMA KABLA YA KUANZA KUFUGA

Mmiliki wa shamba la Ndoto Farm mkoani Iringa, Bw. Hartmut, amewataka wafugaji kuhakikisha wanakuwa na uhakika wa malisho ya mifugo kwa kipindi cha mwaka mzima kabla ya kuanza kufuga, akisisitiza kuwa hatua hiyo ndiyo msingi wa kuongeza tija katika ufugaji.

Bw. Hartmut ametoa kauli hiyo leo, Februari 19, 2026, alipotembelewa na wafugaji kutoka Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga wanaonufaika na Mradi wa Maziwa Faida unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki.

Wafugaji hao, wakiongozana na Mkurugenzi wa Kanda hiyo, Dkt. Zabron Nziku, Mratibu Msaidizi wa Mradi, Watafiti pamoja na Maafisa Ugani kutoka Muheza, wamefanya ziara ya mafunzo kwa baadhi ya wafugaji wa Mkoa wa Iringa kwa lengo la kujifunza kwa vitendo masuala ya ufugaji bora wa ng’ombe wa maziwa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Hartmut alisisitiza kuwa malisho ni uti wa mgongo wa mafanikio katika ufugaji.

“Mifugo ni malisho, usitegemee kupata matokeo ikiwa huna uhakika wa malisho ya mifugo yako, hususani kipindi cha kiangazi. Hakikisha unapanda malisho kwanza ndipo uanze kufuga ili kupata tija katika ufugaji wako,” ameeleza Bw. Hartmut

Kuhusu udhibiti wa magonjwa, Bw. Hartmut aliwahimiza wafugaji kuogesha mifugo yao angalau mara mbili kwa wiki ili kujikinga dhidi ya magonjwa yanayoenezwa na kupe, pamoja na kuzingatia ratiba sahihi ya chanjo.

Kwa upande mwingine Bw. Galus Msekwa ambaye pia ni mmojawapo wa wafugaji waliotembelewa alisema kuwa mafanikio yake yametokana na kuzingatia misingi ya kitaalamu ya ufugaji. Alieleza kuwa uhakikisha ndama wananyonya maziwa ya mama zao ndani ya siku 14 za mwanzo, kisha kuwapa maziwa mbadala kiasi cha lita 10 kwa muda wa miezi mitatu.

“Sasa ng’ombe mmoja shambani kwangu anatoa zaidi ya lita 35 za maziwa kwa siku, jambo ambalo ni faraja kubwa kwangu,” amesema Bw. Msekwa.

Nae, Dkt. Nziku aliwataka wafugaji hao kuyafanyia kazi yote waliyojifunza kwenye ziara hii ili kuongeza uzalishaji na kipato.