Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
MRADI WA MAZIWA FAIDA WAJENGA UWEZO KWA WAFUGAJI WA MUHEZA KUPITIA ZIARA YA MAFUNZO IRINGA NA MBEYA
25 Feb, 2026
MRADI WA MAZIWA FAIDA WAJENGA UWEZO KWA WAFUGAJI WA MUHEZA KUPITIA ZIARA YA MAFUNZO IRINGA NA MBEYA

Mradi wa Maziwa Faida unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland Tanzania na kutekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Sekta ya Kilimo na Chakula ya nchini Ireland (Teagasc), umewezesha ziara ya mafunzo kwa wafugaji 20 kutoka Muheza, mkoani Tanga.

Wafugaji hao ni wanufaika wa mradi huo, ambao unalenga kuwajengea uwezo katika mbinu bora na za kisasa za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Lengo kuu la Mradi wa Maziwa Faida ni kuongeza thamani katika mnyororo wa uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa nchini, kuanzia uzalishaji hadi masoko.

Kupitia ziara hiyo ya mafunzo, wafugaji walipata fursa ya kutembelea wafugaji wenzao pamoja na vyama vya ushirika katika mikoa ya Iringa na Mbeya, ambako walijifunza kwa vitendo mbinu mbalimbali za kisasa za ufugaji.

Miongoni mwa masuala waliyojifunza ni pamoja na uzalishaji na utunzaji bora wa malisho, upandaji na uhifadhi wa vyakula vya mifugo, lishe bora ya ng’ombe wa maziwa, udhibiti wa magonjwa ya mifugo, pamoja na mbinu za uongezaji thamani wa maziwa.

Aidha, walipata elimu kuhusu fursa za masoko na umuhimu wa kuwa na uongozi imara katika vyama vya ushirika ili kuimarisha mafanikio ya wafugaji.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa ziara hiyo, Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Mashariki, Dkt. Zabron Nziku ambae pia ni Msimamizi Mkuu wa Mradi huo aliwataka wafugaji kuhakikisha wanayatumia kikamilifu maarifa na ujuzi walioupata ili kuboresha uzalishaji na kuongeza kipato kupitia ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Kwa upande wao, wafugaji walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema imewafungua macho na kuwapa mbinu mpya za kuboresha shughuli zao. Waliahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo kwa vitendo ili kufikia malengo ya mradi na kuinua sekta ya maziwa katika maeneo yao.