Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
WAZIRI KAKURWA AITAKA BODI YA TALIRI KUSIMAMIA MIRADI YA KIMKAKATI YA UTAFITI WA MIFUGO
10 Aug, 2026
WAZIRI KAKURWA AITAKA BODI YA TALIRI KUSIMAMIA MIRADI YA KIMKAKATI YA UTAFITI WA MIFUGO

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mb), ameielekeza Bodi ya Nne ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuhakikisha inasimamia kwa ufanisi utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha mbari za mifugo, kuimarisha afya ya mifugo, kuongeza uzalishaji wa malisho na mbegu bora za malisho, pamoja na kuhimiza matumizi ya matokeo ya tafiti katika kufanya maamuzi na kuendeleza sekta ya mifugo nchini.

Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa ametoa maelekezo hayo leo Agosti 07, 2026, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Nne ya Wakurugenzi ya TALIRI iliyofanyika katika ukumbi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi jijini Dodoma, ambapo amewataka wajumbe wa Bodi hiyo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, maslahi ya Taifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya mifugo kwa kuimarisha uwezo wa TALIRI kupitia ujenzi wa miundombinu ya utafiti, ununuzi wa vifaa vya kisasa pamoja na kuongeza rasilimali watu, hatua zinazolenga kuiwezesha Taasisi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Pamoja na hayo Mhe. Balozi Dkt. Kakurwa ameitaka Bodi kuweka mkazo katika kuendeleza watafiti wa TALIRI kupitia mafunzo ya mara kwa mara, matumizi ya teknolojia za kisasa, kuimarisha ushirikiano na taasisi za utafiti, vyuo vikuu, sekta binafsi pamoja na wafugaji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nne ya Wakurugenzi ya TALIRI, Prof. Esron Karimuribo, amesema Bodi hiyo imejipanga kuisimamia Taasisi kwa weledi na uadilifu ili kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinatoa majibu ya changamoto zinazowakabili wafugaji na kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya mifugo nchini.

Akitoa taarifa ya Taasisi katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Vitus Komba, amesema Taasisi imeendelea kutekeleza jukumu lake la kufanya utafiti wa mifugo, kuibua teknolojia bunifu na kuzisambaza kwa wafugaji kupitia vituo vyake tisa vilivyopo katika kanda saba za kiikolojia nchini.