Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
RHODES GRASS, MALISHO BORA KWA UZALISHAJI WENYE TIJA KWA MIFUGO
03 Sep, 2026
RHODES GRASS, MALISHO BORA KWA UZALISHAJI WENYE TIJA KWA MIFUGO

Wafugaji nchini wametakiwa kuzingatia uzalishaji na matumizi ya nyasi bora za malisho aina ya Chloris gayana, maarufu kama ‘Rhodes Grass’ kutokana na uwezo wake wa kustawi katika maeneo yenye mvua kidogo, kutoa kiasi kikubwa cha malisho na kuchangia katika kuboresha ukuaji na uzalishaji wa mifugo.

Chloris gayana ni aina ya nyasi inayotumika kwa ajili ya kulisha mifugo na ni miongoni mwa malisho yanayoweza kuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa malisho, hususan katika kipindi cha kiangazi.

Moja ya sifa muhimu za ‘Rhodes Grass’ ni uwezo wake wa kustawi katika maeneo yanayopata mvua kati ya milimita 700 hadi 1,250 kwa mwaka. Sifa hii huifanya kuwa chaguo muhimu kwa wafugaji katika maeneo yenye mvua za wastani au vipindi virefu vya ukame.

‘Rhodes Grass’ inaweza pia kupandwa kwa kuchanganywa na aina mbalimbali za mikunde inayofaa kwa malisho ya mifugo, ikiwemo ‘Stylo, Siratro, Glycine na Tropical Kudzu’

Mchanganyiko wa nyasi na mikunde unaweza kusaidia kuboresha ubora wa malisho na kuongeza upatikanaji wa virutubisho muhimu kwa mifugo, hivyo kusaidia wafugaji kupata lishe yenye uwiano mzuri zaidi. 

Kwa mujibu wa taarifa za uzalishaji, ‘Rhodes Grass’ inaweza kutoa takribani tani 8 hadi 12 za majani makavu (hei) kwa hekta, huku uzalishaji ukiweza kuwa mkubwa zaidi katika maeneo yenye rutuba nzuri ya udongo na kiwango cha kutosha cha mvua.

‘Rhodes Grass’ ni miongoni mwa nyasi zinazofaa kwa ajili ya kutengeneza hei, ambayo ni muhimu katika kuhifadhi malisho kwa matumizi ya mifugo wakati wa kiangazi.

Kwa ubora mzuri wa hei, nyasi inapendekezwa kuvunwa wakati inapoanza kuchanua maua. Wakati huo, bado huwa na ubora mzuri wa lishe na mifugo huweza kupenda zaidi ikilinganishwa na nyasi iliyochelewa kuvunwa na kuwa ngumu.

Nyasi hii huwa na kiwango cha protini kinachokadiriwa kufikia asilimia 5 hadi 6 inapofikia hatua ya kuchanua maua. Mifugo hupendelea kula ‘Rhodes Grass’ hasa inapokuwa changa na haijakomaa kupita kiasi.

Lishe bora ni msingi wa uzalishaji wenye tija katika sekta ya mifugo. Matumizi ya ‘Rhodes Grass’ kama sehemu ya lishe ya mifugo yanaweza kusaidia kuboresha ukuaji na hali ya mwili wa mifugo na kuchangia katika uzalishaji wa nyama na maziwa, hasa inapounganishwa na vyanzo vingine vya virutubisho kulingana na mahitaji ya mnyama.

Ili kunufaika zaidi na ‘Rhodes Grass’ wafugaji wanashauriwa kuzingatia uchaguzi wa mbegu bora, maandalizi sahihi ya shamba, upandaji kwa wakati, udhibiti wa magugu, matumizi sahihi ya mbolea na uvunaji katika hatua inayofaa.

Hivyo, wafugaji wanahimizwa kuzalisha na kuhifadhi malisho ya kutosha kabla ya kuanza kwa msimu wa kiangazi ili kuhakikisha mifugo inaendelea kupata chakula kwa mwaka mzima.

Wafugaji wanahimizwa kulima malisho bora, kuyahifadhi kwa wakati na kuyatumia kwa usahihi ili kuongeza tija na kupunguza changamoto ya upungufu wa malisho.

RHODES GRASS — Malisho Bora, Mifugo Yenye Tija Zaidi.