TALIRI YATAKIWA KUJUMUISHA MABADILIKO YA TABIANCHI KATIKA TAFITI ZA MIFUGO
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Fabian Madele, ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuhakikisha kuwa masuala ya mabadiliko ya tabianchi yanajumuishwa katika tafiti zake ili kuimarisha uwezo wa sekta ya mifugo kukabiliana na athari za mabadiliko hayo.
Dkt. Madele ametoa maelekezo hayo leo, tarehe 21 Oktoba 2026, alipotembelea Makao Makuu ya TALIRI kwa ajili ya kukutana na Timu ya Menejimenti na kujadili utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Madele amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi katika kubuni na kutekeleza programu na miradi ya utafiti, akieleza kuwa hali hiyo inahitaji mikakati madhubuti itakayosaidia kupunguza athari zake kwa mifugo na shughuli za ufugaji.
“Mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuongeza ukali wa athari za matukio ya hali mbaya ya hewa, ikiwemo mvua kubwa na mafuriko yanayoweza kujitokeza wakati wa El Nino kama ambavyo tumekuwa tukitangiziwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). Hali hii inasisitiza umuhimu wa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi katika kupanga na kutekeleza tafiti za mifugo, hususani katika kubuni teknolojia zinazosaidia mifugo kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa” amesema Dkt. Madele.
Aidha, Dkt. Madele ameitaka TALIRI kuendelea kufanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wafugaji, akisisitiza umuhimu wa tafiti hizo ni kuleta suluhisho zinazotekelezeka na kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya mifugo nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Komba, amesema Taasisi itaendelea kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya kufanya utafiti, kutathmini na kusambaza teknolojia bora za mifugo.
Prof. Komba ameongeza kuwa juhudi hizo zitaendelea kulenga upatikanaji wa teknolojia na mbinu bora za ufugaji zitakazosaidia kuongeza uzalishaji, kupunguza changamoto zinazowakabili wafugaji na kuimarisha uwezo wa sekta ya mifugo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
