Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI YAANZA UTAFITI WA KUBORESHA NG’OMBE AINA YA MPWAPWA
20 Oct, 2026
TALIRI YAANZA UTAFITI WA KUBORESHA NG’OMBE AINA YA MPWAPWA

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imeendelea kutekeleza programu ya utafiti inayolenga kuboresha ng’ombe aina ya Mpwapwa ili kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka wastani wa lita tano hadi nane kwa siku, hadi kufikia lita 15, kwa lengo la kukidhi mahitaji ya wafugaji na kuongeza tija katika sekta ya maziwa nchini.
 
Hatua hiyo inatokana na shauku ya wananchi, hususan wafugaji, ya kutaka kuona ng’ombe aina ya Mpwapwa, ambaye amezalishwa na TALIRI, akiendelea kuboreshwa ili kuongeza uzalishaji wa maziwa huku akihifadhi sifa zake muhimu za kustahimili mazingira ya ukame na magonjwa.
 
Akielezea utekelezaji wa programu hiyo, Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Kati, Dkt. Mwemezi Kabululu, amesema utafiti huo unalenga kupata ng’ombe chotara mwenye uwezo mkubwa wa kuzalisha maziwa ikilinganishwa na ng’ombe wa Mpwapwa.
 
Amesema kuwa katika kutekeleza programu hiyo, TALIRI kupitia kituo chake cha utafiti kilichopo Mpwapwa (TALIRI Mpwapwa) mkoani Dodoma, imefanya uzalishaji kwa njia ya upandishaji wa chupa (artificial insemination) kwa ng’ombe aina ya Mpwapwa kwa kutumia mbegu za ng’ombe aina ya Danish Red, ambaye ni ng’ombe wa maziwa kutoka nchini Denmark.
 
Kwa mujibu wa Dkt. Kabululu, mpango huo unalenga kuzalisha aina mbili za ng’ombe chotara; mmoja atakayekuwa na kiwango kikubwa zaidi cha vinasaba vya Danish Red na mwingine atakayekuwa na kiwango kikubwa zaidi cha vinasaba vya Mpwapwa.
 
Ameeleza kuwa mkakati huo unalenga kukidhi mahitaji ya makundi mbalimbali ya wafugaji kwa kuzingatia uwezo wao wa kuhudumia ng’ombe, hususan mahitaji ya malisho, lishe na mazingira ya ufugaji.
 
“Matokeo ya awali ya utafiti yameonesha kuwa katika kizazi cha kwanza tumepata ng’ombe mwenye uwezo wa kuzalisha hadi lita 15 za maziwa kwa siku,” amesema Dkt. Kabululu.
 
Ameongeza kuwa kuboresha ng’ombe aina ya Mpwapwa kunalenga kuongeza uzalishaji wa maziwa bila kupoteza sifa za msingi zilizozingatiwa wakati wa kumzalisha, ambazo ni pamoja na kustahimili mazingira ya ukame, kuhimili magonjwa na kuweza kuendana na mifumo ya ufugaji inayotumika katika maeneo mbalimbali nchini.
 
Ng’ombe aina ya Mpwapwa alizalishwa kwa lengo la kukidhi mahitaji ya wafugaji wanaofuga katika maeneo yenye hali ya ukame, hususani Kanda ya Kati. Mbali na kustahimili mazingira magumu, ng’ombe huyo ana uwezo wa kutumika kwa ajili ya uzalishaji wa nyama na maziwa, huku akiwa na ukuaji wa haraka na uwezo wa kufikia uzito mkubwa ndani ya muda mfupi.
 
Aidha, ng’ombe huyo ana uwezo wa kuzalisha wastani wa lita tano hadi nane za maziwa kwa siku, kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na ng’ombe wengi wa asili wanaozalisha takribani lita moja hadi mbili kwa siku.
 
Sifa nyingine muhimu ya ng’ombe aina ya Mpwapwa ni mahitaji yake madogo ya matunzo ikilinganishwa ya ng’ombe wengi wa kisasa, hali inayomuwezesha kufugwa hata katika mifumo ya ufugaji wa kawaida, mradi apatiwe huduma muhimu za mifugo kama lishe na maji.
 
Kupitia programu hiyo ya utafiti, TALIRI inalenga kuongeza tija katika uzalishaji wa maziwa, kuboresha kipato cha wafugaji na kuchangia upatikanaji wa maziwa nchini, huku ikiendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za utafiti zinazozingatia mazingira na mahitaji halisi ya wafugaji wa Tanzania.