WAFUGAJI WASHAURIWA KUTUMIA VIRUTUBISHO VYA ASILI KWENYE UFUGAJI

Wafugaji nchini wameshauriwa kutumia virutubisho vya asili katika ufugaji wao ili kuleta tija na kupunguza matumizi ya kemikali kwa mifugo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Erick Vitus Komba wakati akitambulisha bidhaa za virutubisho asilia mbele ya waandishi wa habari ndani ya banda la taasisi hiyo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ‘Nanenane’ yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
“Mwelekeo wa Dunia kwa sasa ni kuzalisha vyakula bila kutumia kemikali kwa wingi kwani matumizi makubwa ya kemikali kwa vyakula na wanyama yanaleta madhara makubwa kwa binadamu” amesema Prof. Komba.
Bidhaa hizo hazina kemikali bali ni virutubisho vya asili ambapo mnyama akitumia zina uwezo wa kuvuta bakteria wa faida ambao wanakuwa na kazi ya kuongeza kinga ya mwili kwa mnyama na kusaidia mmeng’enyo wa chakula.
“Mfugaji akitumia bidhaa hizi wanyama watakuwa kwa haraka na kupunguza utumiaji wa madawa yenye kamikali” Amesema Prof.Komba.
Kwa upande wake Bw. Paruku Emmanuel mzalishaji na muuzaji wa bidhaa hizo zinawezesha mifugo kukua vizuri na mazao kustawi kutoka nchini Indonesia amesema kuwa bidhaa hizo zimefanyiwa utafiti na TALIRI kwa muda wa miaka mitatu na zimeleta matokeo chanya kwa mazao na mifugo.
“Teknolojia hizi zimefanyiwa utafiti na TALIRI kwa wanyama kama kuku na ng’ombe na zimeleta matokeo chanya, ukitumia bidhaa hizi mnyama hatokuwa na kemikali au mabaki ya madawa mwilini hivyo kupelekea kuwa na usalama na ubora wa nyama zinazoliwa na binadamu kwani matumizi makubwa ya kemikali kwa mifugo huleta madhara kwa binadamu, wito wangu kwa wafugaji ni kutumia bidhaaa zetu ili kuongeza tija kwenye ufugaji wao” Amesema Bw. Paruku.