Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
FAHAMU UMUHIMU WA MAABARA YA LISHE YA WANYAMA
10 Oct, 2024
FAHAMU UMUHIMU WA MAABARA YA LISHE YA WANYAMA

Katika kuhakikisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) inatekeleza vyema jukumu lake la kuzalisha teknolojia bora za mifugo zinazoibuliwa na taasisi hiyo, ikiwemo mbari bora za mifugo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na mazao mengine ya mifugo pamoja na elimu ya mbegu bora za malisho na vyakula vya mifugo taasisi hiyo inajivunia kuwa na maabara ya lishe ya wanyama ambayo inatumika kupima ubora wa chakula cha mifugo.

Akiongea, Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku ameeleza kuwa huwezi kufanya sayansi ya wanyama bila kuwa na maabara hiyo kwani ili mnyama aweze kuwa na afya na mazao yake yaweze kuwa bora ni muhimu chakula anachopewa mnyama kipimwe na kitathiminiwe ili kujua ubora wake.

“Lakini pia kujua yapi ni malisho bora kwa wanyama ni lazima kutumia maabara hii” aliongeza Dkt. Nziku.

Dkt. Nziku ameongeza kuwa kupitia maabara hiyo vijana kutoka vyuo mbalimbali nchini, vya kati na vyuo vikuu, watapata fursa ya kujifunza na kuelimika juu ya matumizi ya maabara hiyo muhimu kwa wanyama na hatimae kuwa wataalamu wazuri wa kulisaidia Taifa hili juu ya chakula cha mifugo.

Aidha, Dkt. Nziku ameipongeza Serikali kwa ujenzi wa maabara hiyo ambayo pia imeboreshwa kupitia mradi wa maziwa faida unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania ambao umewezesha kuboresha miundombinu ya maabara hiyo, ununuzi wa vifaa pamoja na kusafirisha wataalamu wa taasisi hiyo kwenda nchini Ireland kwa ajili ya kujifunza jinsi ya kuendesha na kujua vifaa muhimu vinavyopaswa kuwepo kwenye maabara hiyo.

Kwa upande wake Ndg. Valentino Urassa Mtafiti Mwandamizi wa TALIRI Tanga anayesimamia maabara hiyo ameeleza kuwa maabara hiyo imekuwa ikipokea sampuli mbalimbali za malisho kutoka kwenye mashamba ya taasisi pamoja na mashamba ya wafugaji ili kuweza kuzichakata na kujua kilichopo kwenye malisho hayo ya wanyama, pamoja na kuangalia mabaki ya madawa aliyopewa mnyama kama yapo kwenye maziwa.