Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI YAPONGEZWA KWA UTOAJI WA ELIMU BORA YA UFUGAJI
02 Aug, 2025
TALIRI  YAPONGEZWA KWA  UTOAJI WA ELIMU BORA  YA UFUGAJI

 

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald G Mweli ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa utoaji wa elimu ya ufugaji bora kwa wafugaji na wadau mbalimbali wa mifugo.

Pongezi hizo amezitoa leo tarehe 02/08/2025 alipotembelea banda la taasisi hiyo lililopo ndani ya viwanja vya Nzuguni jijini Dar es salaam yanapoendelea Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ‘Nanenane’ yakiwa na kaulimbiu isemayo ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’

Mbali na pongezi hizo Mweli ameitaka Taasisi hiyo kuendelea kusambaza teknolojia bora za mifugo zinazozalishwa na taasisi hiyo kwa wafugaji kote nchini.

“Nimefurahishwa na mambo mazuri yanayofanywa na taasisi hii sasa ni wakati wa kuongeza nguvu ya kuhakikisha teknolojia bora za mifugo zinawafikia wafugaji ili kuongeza tija ya ufugaji” Ameongeza Mweli.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Erick Komba amesema katika maonesho hayo Taasisi imejipanga kutoa elimu juu ya teknolojia bora za mifugo zilizozalishwa na taasisi hiyo ikiwemo malisho ya mifugo, mbari bora za mifugo na vyakula vya ziada vya mifugo.

Sambamba na hayo Prof. Komba ameeleza kuwa wafugaji na wadau mbalimbali wa mifugo wanapata fursa ya kujifunza na kujionea kifaa maalumu kilichotengenezwa kwa ajili ya kuwezesha matumizi rahisi ya kupima uzito, kutoa dawa, kuweka hereni na matibabu ya mifugo kwa usalama zaidi.

“Kifaa hicho kinatoa fursa kwa wafugaji kuwa na njia ya rahisi ya kutunza taarifa muhimu za mifugo ikiwemo kujua uzito wa mifugo yao na hivyo kufanikiwa kujua maendeleo ya mifugo kwani sasa mwelekeo wa Wizara ni kuhakikisha mifugo inauzwa kutokana na uzito wake” ameongeza Prof. Komba.

Pamoja na hayo wafugaji wanaendelea kupatiwa elimu ya kuogesha mifugo kwa kutumia kifaa rahisi cha kuogeshea ambacho mfugaji wa hali ya kawaida anaweza kumudu kuwa nacho