BODI YA WAKURUGENZI YAIPONGEZA TALIRI KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UTAFITI

Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) leo tarehe 11/04/2025 imefanya ziara ya kukagua miradi ya utafiti inayotekelezwa katika kituo cha TALIRI Mpwapwa.
Katika ziara hiyo iliyofuatiwa na kikao cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025 bodi hiyo imepata fursa kutembelea, shughuli za utafiti zinazoendelea kituoni hapo ikiwemo mradi wa utafiti wa mbuzi, ng’ombe na uzalishaji wa malisho.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, mwenyekiti wa bodi hiyo Prof. Sebastian Chenyambuga ameipongeza TALIRI kwa kazi nzuri ya uzalishaji wa teknolojia bora za mifugo kituoni hapo na kuishukuru Serikali kwa kuiwezesha taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake ya shughuli za utafiti kwa maslahi ya wafugaji nchini.
“Nawakumbusha wafugaji kuchangamkia fursa ya matokeo ya utafiti ili mnufaike na ufugaji wenu ikiwemo teknolijia ya mbegu za malisho na mbari bora za mifugo kwa ufugaji wenye tija na hatimae kujikwamua kiuchumi” Amesema Prof. Chenyambuga.
Akiwakilisha wajumbe wa bodi hiyo, Ndg. Yohana Kubini, amewataka wafugaji kujua umuhimu wa TALIRI katika upatikanaji wa mazao ya mifugo yenye tija ikiwemo maziwa mengi ambayo hutokana na mbari bora za mifugo zilizofanyiwa utafiti wa kina na watafiti wa Taasisi hiyo akiwemo Ng’ombe aina ya Mpwapwa.
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Prof. Erick Komba amesema mkakati wa Taasisi ni kuhakikisha teknolojia bora za mifugo zinaendelea kusambazwa kwa wafugaji ili kuongeza tija ya ufugaji nchini.
Prof. Komba ameongeza kuwa taasisi imepokea maelekezo yaliyotolewa na bodi hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi kwani kati ya maelekezo hayo ambayo yamelenga kuongeza tija ya ufugaji nchini mengi yapo kwenye hatua ya utekelezaji.
Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya bodi ambapo kila robo mwaka hukutana kujadili maendeleo ya miradi ya utafiti inayotekelezwa na taasisi hiyo pamoja na kutoa ushauri katika kuboresha shughuli mbalimbali za taasisi ili kufikia malengo iliyojiwekea.