Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TDGG KUTUMIA TEKNOLOJIA NA TAKWIMU KUHARAKISHA UBORESHAJI WA NG'OMBE WA MAZIWA
25 Jun, 2026
TDGG KUTUMIA TEKNOLOJIA NA TAKWIMU KUHARAKISHA UBORESHAJI WA NG'OMBE WA MAZIWA

Mradi wa Kuboresha Vinasaba vya Ng’ombe wa Maziwa katika Ukanda wa Kitropiki (TDGG) umeweka mikakati mbalimbali ya kisayansi na kiteknolojia itakayosaidia kuendelea kuongeza tija na ushindani katika sekta ya maziwa kupitia uboreshaji endelevu wa vinasaba vya mifugo.

Hayo yameelezwa na Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Bw. Gilbert Msuta, wakati wa warsha iliyowakutanisha wadau wa Sekta ya Mifugo inayoendelea katika Hoteli ya Panama Mkoani Kilimanjaro, iliyolenga kujadili uwezo na matumizi ya mfumo wa Mradi wa TDGG pamoja na kuweka mikakati ya kuendeleza na kupanua matumizi ya mfumo huo ili kuwafikia wafugaji na wadau wengi zaidi.

Bw. Msuta amesema kuwa mradi huo unalenga kuwawezesha wafugaji wadogo kupata mifugo yenye tija kubwa na inayoweza kuhimili mazingira ya maeneo yao kupitia mifumo endelevu ya uboreshaji wa mifugo, ukusanyaji wa takwimu na utoaji wa mrejesho na huduma za ushauri.

“Katika kufanikisha malengo hayo, TDGG imeweka mkakati wa kuhakikisha kunakuwepo mifumo sahihi ya kuchagua ng’ombe bora kwa kuzingatia vinasaba sahihi vyenye uwezo mkubwa wa kijenetiki huku ikihakikisha mifugo inayochaguliwa inaendana na mazingira ya eneo husika,” amesema Msuta.

Aidha, Bw. Msuta amesema kuwa mfumo wa kidijitali wa kurekodi utendaji wa mifugo shambani utatumika kufuatilia taarifa muhimu zitakazosaidia kufanya tathmini za kijenetiki na uchaguzi wa mifugo bora kwa kutumia teknolojia za ‘genomics’

Vilevile Bw. Msuta, ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo pia utazingatia upimaji wa viashiria muhimu vinavyojumuisha uzalishaji wa maziwa, uzazi, afya na ustahimilivu wa mazingira, pamoja na kiwango cha uzalishaji wa gesi ya methane na athari zake kwa mazingira.

Ameongeza kuwa TDGG itaendelea kuimarisha mifumo ya ugani wa kidijitali na utoaji wa mrejesho kwa wafugaji sambamba na kuendeleza ushirikiano kati ya sekta za Umma na sekta binafsi ili kuhakikisha matokeo ya mradi huo yanakuwa endelevu.

Mradi wa TDGG unatekelezwa na TALIRI kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) kwa ufadhili wa Wakfu wa Bill & Melinda Gates.