Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
WADAU WA TDGG WAWEKA MIKAKATI YA UTEKELEZAJI NA KUIMARISHA UWAJIBIKAJI WA PAMOJA
26 Jun, 2026
WADAU WA TDGG WAWEKA MIKAKATI YA UTEKELEZAJI NA KUIMARISHA UWAJIBIKAJI WA PAMOJA

Washiriki wa Warsha ya Mradi wa Kuboresha Vinasaba vya Ng’ombe wa Maziwa katika Ukanda wa Kitropiki (TDGG) iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Panama mkoani Kilimanjaro leo, Juni 25, 2026, wamehitimisha warsha hiyo kwa kuweka mikakati ya utekelezaji, kubainisha vipaumbele na kuainisha majukumu ya kila mdau ili kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa kwa ufanisi.

Katika siku ya mwisho ya warsha hiyo, washiriki walifanya zoezi la pamoja la kuboresha na kuratibu majukumu ya wadau mbalimbali, sambamba na kuweka ratiba na muda maalum wa utekelezaji wa shughuli zilizokubaliwa.

Aidha, washiriki walijadili maeneo ya kipaumbele yatakayosaidia kuimarisha matumizi ya takwimu, teknolojia za kidijitali na ushirikiano baina ya taasisi mbalimbali katika kuboresha mfumo wa uzalishaji wa maziwa nchini.

Warsha hiyo ilihitimishwa kwa zoezi la utoaji wa ahadi za utekelezaji, ambapo kila mdau alieleza jukumu lake katika kusukuma mbele utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa. Hatua hiyo inalenga kuimarisha uwajibikaji wa pamoja na kuhakikisha mfumo wa TDGG unatumika kwa kiwango kikubwa zaidi.

Washiriki wa warsha hiyo ni pamoja na watunga sera, taasisi mbalimbali za Serikali, watafiti, washirika wa maendeleo, wafugaji wadogo na wa kibiashara, vyama vya ushirika, wasindikaji wa maziwa, maafisa ugani pamoja na wasambazaji wa pembejeo za mifugo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mratibu wa Mradi wa TDGG kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), Dkt. Eliamoni Lyatuu, na Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Bw. Gilbert Msuta, waliwashukuru washiriki wote kwa michango yao, wakieleza kuwa mawazo na mapendekezo yaliyotolewa yatachangia kuongeza tija katika mnyororo wa thamani wa sekta ya maziwa nchini.

Warsha hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa TDGG unaotekelezwa na TALIRI kwa kushirikiana na ILRI, kwa ufadhili wa Wakfu wa Bill & Melinda Gates, ukiwa na lengo la kuimarisha mifumo ya uboreshaji wa vinasaba vya ng’ombe wa maziwa kupitia matumizi ya takwimu, teknolojia za kidijitali na mbinu za kisasa.