Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
MKUU WA MKOA WA TANGA AIPONGEZA TALIRI KWA TAFITI ZENYE TIJA
24 Feb, 2025
MKUU WA MKOA WA TANGA AIPONGEZA TALIRI KWA TAFITI ZENYE TIJA

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki kwa kufanya tafiti zenye tija zinazolenga kuinua uchumi wa wananchi zikiwemo tafiti za mbari bora za mifugo, vyakula vya mifugo na malisho ya mifugo.

Dkt. Batilda ametoa pongezi hizo leo tarehe 29/01/2025 alipotembelea ofisi za kanda hiyo ambayo kituo chake kipo mkoani hapo kwa lengo la kujionea shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo kituoni hapo hususani za Mradi wa Maziwa Faida.

Pamoja na pongezi hizo Dkt. Batilda ameitaka taasisi hiyo kuendelea kusambaza kwa wingi teknolojia zake hususani za malisho ili kusaidia kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TALIRI Kanda ya Mashariki Dkt. Zabron Nziku ameeleza kuwa kupitia mradi wa maziwa faida taasisi imefanikiwa kuwafikia wafugaji 2,334 wilayani Muheza kwa kuwapatia elimu za ufugaji bora kwa lengo la kuboresha ufugaji wao.

Aidha, Dkt. Nziku ameeleza kuwa mbali na mafunzo mbalimbali kwa wafugaji, mradi umefanikiwa kuanzisha shamba darasa kwa ajili ya kuwapa fursa wafugaji kwenda kujifunza kwa vitendo juu ya upandaji, utunzaji, uvunaji, na ulishaji wa malisho yaliyoboreshwa.

Dkt. Nziku ameendelea kueleza kuwa mradi wa maziwa faida umelenga kuinua wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa kuhakikisha wanapata weledi juu ya ufugaji bora na hivyo kuwezesha kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani wa ng’ombe wa maziwa.

Mradi wa Maziwa Faida kwa sasa unatekelezwa mkoani Tanga ndani ya Wilaya ya Muheza.