BARAZA LA WAFANYAKAZI TALIRI LAPITISHA MAKADIRIO YA BAJETI YA 2025/2026

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Masoko na Uzalishaji Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Steven Maiko amesema kwa mwaka ujao wa fedha wa 2025/2026 wizara hiyo imeendelea kutenga fedha za maendeleo kwa ajili ya kuiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwa itaendelea kuhakikisha kuwa taasisi hiyo inapata bajeti ya kutosha.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 14/02/2024 katika kikao cha 6 cha baraza kuu la wafanyakazi la TALIRI kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya African Dreams uliopo mkoani Dodoma kilicholenga kujadili na kupitisha Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Steven ameendelea kueleza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini mchango wa tafiti zinazofanywa nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick Komba amesema TALIRI kwa mwaka ujao wa fedha 2025/2026 imejipanga kuhakikisha kuwa vipaumbele vya utekelezaji wa bajeti ya mwaka huo vinatekelezwa kwa weledi kwa maslahi ya wafugaji, wadau wa mifugo na Serikali kwa ujumla.
Akiwasilisha Taarifa ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Meneja Sehemu ya Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini TALIRI Bw. Benard Francis amesema katika mwaka ujao wa fedha taasisi inakadiria kukusanya na kupokea mapato yenye jumla ya Tsh 16,063,058,427.00 ambayo ni sawa na ongezeko la 19.8% ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2024/2025 ambayo ni Tsh 12,883,550,415.00.
Benard ameendelea kueleza kuwa mapato na matumizi ya bajeti hiyo yamegawanyika katika vyanzo mbalimbali kwa mchanganuo ufuatao Tsh 1,642,841,000.00 mapato ya ndani ya taasisi, Tsh 1,595,000,000.00 ruzuku ya matumizi mengineyo, Tsh 5,779,412,856.00 Mishahara, Tsh 7,045,804,571.00 ikiwa ni fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Aidha, Benard ameeleza kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo utazingatia kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali ya vipaumbele ikiwemo malisho na mbegu za malisho, mbari za mifugo, vyakula vya mifugo, afya ya mifugo, virutubisho asilia, tabia na haki za mifugo na kuwajengea uwezo wataalamu wa taasisi hiyo.