Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI KUENDELEZA MRADI WA BBT.
23 Sep, 2025
TALIRI KUENDELEZA MRADI WA BBT.

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) yajipanga kuendeleza utekelezaji wa Programu ya Jenga Kesho Iliyobora (Building Better Tommorow - BBT) kupitia Mradi wa BBT Project I unaolenga kuwezesha vijana na wanawake wa Kitanzania kuwa wajasiriliamali wenye mafanikio kwenye kilimo na ufugaji wa kibiashara.

Akiongea leo tarehe 02/09/2025 namna mradi huo utatekelezwa kitaifa kwa upande wa sekta ya Kilimo na Mifugo katika kikao cha kuelezea utekelezaji wa mradi kilichofanyika TALIRI Bi. Vumilia Zikankuba Mratibu wa Mradi amesema mradi umelenga kuwezesha vijana katika kilimo biashara, kuendeleza kilimo cha vitalu (Block farming) kinachostahimili mabadiliko ya tabia ya nchi, biashara ya unenepeshaji wa mifugo na kilimo cha malisho.

Bi. Zikankuba ameendelea kueleza kuwa mradi utawezesha vijana na ushiriki wa sekta binafsi kupitia upatikanaji wa mikopo ya riba nafuu na kuwezesha dhamana za kupata mikopo hiyo kutoka taasisi za fedha.

“Pamoja na hayo mradi umepanga kuwezesha vijana 11,000 watakaoshiriki katika shughuli za kilimo na ufugaji kupitia vituo atamizi na ajira za moja kwa moja 150,000 zitatengenezwa kupitia mashamba yenye ukubwa wa ekari 43,500” Ameongeza Bi.Zikankuba.

Vilevile, Bi. Zikankuba ameeleza kuwa TALIRI itatekeleza mradi huo kwa kuwafundisha vijana juu ya shughuli za unenepeshaji wa mbuzi na kilimo cha malisho kibiashara kupitia kituo cha utafiti cha TALIRI Kongwa.

Katika kipindi hiki cha utekelezaji mradi utawezesha ukarabati wa jengo la ofisi, ujenzi wa nyumba za malazi, ukumbi wa mafunzo, mabanda ya mifugo yenye uwezo wa kubeba mbuzi 15,000 kwa pamoja, josho, sehemu ya kutolea matibabu kwa mifugo na ghala la kuhifadhia malisho.

Pamoja na hayo mradi utawezesha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo mfumo wa ‘center pivot’ mabwawa ya kukusanyia maji, matenki ya kuhifadhia maji na uchimbaji wa visima virefu ndani ya kituo cha TALIRI Kongwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI Prof. Erick Komba amesema Taasisi imejipanga kutekeleza mradi huo kwa ufanisi ili kufikia malengo ya mradi na hivyo kuwezesha mnyororo wa thamani kwenye ufugaji.