Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI KUENDELEZA MKAKATI WA KUSAMBAZA TEKNOLOJIA BORA ZA MIFUGO
03 Oct, 2025
TALIRI KUENDELEZA MKAKATI WA KUSAMBAZA TEKNOLOJIA BORA ZA MIFUGO

Katika jitihada za kuendelea kusambaza teknolojia bora za mifugo watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) wakiongozwa na Meneja wa Sehemu ya Uhaulishaji wa Teknolojia wa Taasisi hiyo Bw. Gilbert Msuta wamekabidhi madume mawili ya mbuzi aina ya Malya kwa kikundi cha wafugaji kilichopo wilayani Chamwino Kata ya Segala, Kijiji cha Segala. 

Makabidhiano hayo yamefanyika baada ya kikundi hicho kinachoitwa ‘Malya Goat Association’ kinachojishughulisha na ufugaji wa mbuzi aina ya Malya kuleta maombi ya kununua mbuzi hao waliozalishwa na TALIRI kwa lengo la kuboresha mbuzi wao.

Taasisi kwa kuunga mkono jitihada za kikundi hicho cha wafugaji iliamua kupeleka mbuzi hao katika banda wanalofugia wafugaji hao kwa lengo  kuwashauri na kuwapatia elimu ya juu ya ufugaji bora.

Akizungumza wakati wa kukabidhi madume hayo Meneja Msuta amewataka wafugaji hao kuweka utaratibu maalumu wa kusimamia uzalianaji wa mbuzi hao ili kuepuka ndugu kuzaliana wao kwa wao kwani kitendo hicho hupelekea uzalishaji wa mifugo hiyo kushuka.

Aidha, Meneja Msuta amewataka wanakikundi hao kuzingatia utoaji wa chanjo na kuwashauri kumtumia Afisa Mifugo wa Kata hiyo ili mbuzi hao wachanjwe kwa wakati na kuhakikisha wanafanya maandalizi ya shamba kwa ajili ya kustawisha malisho wakati wa masika.

Kadhalika, Meneja Msuta ameongeza kuwa TALIRI ipo tayari kufanya ufuatiliaji wa karibu kwa kikundi hicho, ili kuhakikisha mbuzi wanaozaliwa wanakuwa na viwango stahiki vinavyokidhi soko kwa kuwapatia elimu ya ustawishaji wa malisho na ufugaji bora wa mbuzi na kuwa milango ya taasisi ipo wazi muda wote kuwapokea kwa ajili ya mafunzo zaidi.

Mwisho mwenyekiti wa kikundi hicho Bw. Saidi Kajeku, kwa niaba ya wanakikundi ameeleza kuwa wanaishukuru TALIRI na kufurahishwa na jitihada walizozifanya kuwasilisha madume hayo na ameahidi kuwatunza na kufuata maelekezo ya watafiti kwani upatikanaji wa mbuzi hao utaenda kuboresha uzalishaji wa mbuzi wao.