WATUMISHI WA TALIRI WAJENGEWA UELEWA WA AFYA, KUBORESHA UFANISI KAZINI
Katika hatua ya kuimarisha ustawi wa watumishi na kuongeza tija kazini, watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Makao Makuu wamepatiwa mafunzo ya afya, yakilenga magonjwa ya kuambukiza, yasiyoambukiza pamoja na afya ya akili.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea watumishi juu ya uelewa wa namna ya kujikinga na magonjwa kwa kubadili mtindo wa maisha, kufanya uchunguzi wa afya mapema na kuzingatia lishe bora.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Dkt. Salma Gwasa kutoka Kituo cha Afya cha Makole alisema magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, kisukari na shinikizo la damu yanaweza kudhibitiwa iwapo kila mtu atabadili mtindi wa maisha.
“Kubadili mtindo wa maisha ni muhimu ikijumuisha kuzingatia lishe bora, mazoezi ya mwili na kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi na kufanya uchunguzi wa afya mapema kunaweza kuokoa maisha,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa watumishi wanapaswa kupunguza matumizi ya chumvi na sukari nyingi, na kuongeza ulaji wa vyakula vyenye virutubisho kama mbogamboga na nafaka zisizokobolewa. Pia alihimiza kufanya mazoezi kwa angalau dakika 20 kwa siku ili kulinda afya.
Kwa upande wa afya ya akili, Dkt. Grace Isack kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe alieleza kuwa changamoto hiyo ni kubwa na huathiri moja kwa moja utendaji kazi.
“Kati ya watu wanne, mmoja anaweza kuwa na changamoto ya afya ya akili. Ni muhimu kutambua dalili za magonjwa ya akili mapema na kutafuta msaada wa kitaalamu badala ya kukimbilia imani potofu au tabia hatarishi,” alisema.
Dkt. Grace alisisitiza umuhimu wa kudumisha uwiano kati ya kazi na maisha binafsi, pamoja na kujenga utamaduni wa kuzungumza na wataalamu pale msongo wa mawazo unapoongezeka.
Pamoja na mafunzo hayo wafanyakazi hao walipata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ya kiutumishi yakiwemo utafiti, utawala pamoja na haki za watumishi wa Umma.
