WAZIRI MKUU AHAMASHISHA KILIMO CHA MALISHO KUIMARISHA SEKTA YA MIFUGO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewataka wafugaji nchini kuwekeza katika kilimo cha malisho ya mifugo ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa malisho na kupunguza migogoro ya matumizi ya ardhi inayojitokeza kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Mhe. Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo, Juni 19, 2026, wakati akifungua Maonesho na Mnada wa Kimataifa wa Mifugo yaliyofanyika katika Ranchi ya Mbogo, Wilaya ya Chalinze, Mkoa wa Pwani. Akizungumza katika hafla hiyo, amesema kuwa uhaba wa malisho ni moja ya changamoto kubwa zinazokwamisha maendeleo ya sekta ya mifugo nchini, hivyo amewahimiza wafugaji na wadau wa sekta hiyo kutumia maonesho hayo kujifunza teknolojia za kisasa za ufugaji, kilimo cha malisho pamoja na matumizi ya mbegu bora za mifugo ili kuongeza tija, uzalishaji na mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa. “Nitumie fursa hii kuwahimiza wadau wote wa mifugo nchini kutumia maonesho haya kujifunza matumizi ya teknolojia za kisasa za ufugaji na kilimo cha malisho ili kuongeza uzalishaji na kukuza biashara ya mifugo kupitia minada inayofanyika sambamba na maonesho haya,” amesema Mhe. Dkt. Mwigulu. Aidha, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na TAMISEMI kutenga na kusimamia maeneo ya malisho kwa ajili ya kuhakikisha matumizi bora na endelevu ya ardhi. Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema lengo kuu la maonesho hayo ni kujenga mfumo imara wa biashara ya mifugo na mazao yake kwa kuwakutanisha wafugaji, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa sekta ya mifugo ili kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora za ufugaji na kupanua fursa za masoko ndani na nje ya nchi. Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Ranchi ya Mbogo ambao ni waandaaji wa maonesho hayo ameipongeza Serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwezesha ufugaji wenye tija na ameitaka kuendelea kuweka mazingira rafiki ili kuwezesha vijana kuwekeza katika Sekta ya Mifugo na hivyo kukuza uchumi wapi na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla. TALIRI inashiriki Maonesho hayo
