WATAALAMU TALIRI WAPATIWA ELIMU YA MAGONJWA SUGU
Wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) leo tarehe 19/11/2024 wamepatiwa elimu juu ya magonjwa sugu yasiyoambukiza ukiwemo ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, kansa, selimundu na kiharusi pamoja na Virusi Vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI lengo ikiwa ni kuwakumbusha kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa hayo.
Akielezea Dkt. Mukhsin Chikota kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma amesema magonjwa yasiyoambukiza yanasababishwa na mtindo wa maisha wa kutozingatia lishe bora, msongo wa mawazo, kutofanya mazoezi, unywaji wa pombe uliopitiliza, uvutaji wa sigara na kutokunywa maji kwa kiwango kinachotakiwa.
Lakini pia Dkt. Chikota ameeleza kuwa VVU huambukizwa kwa kushiriki ngono zembe, kuchangia vitu vyenye ncha kali, kushiriki tendo la ndoa kinyume na maumbile na kuchangia damu ya mtu mwenye maambukizi.
Aidha, Dkt. Chikota ameeleza kuwa ni vyema kujikinga dhidi ya magonjwa hayo kwa kuacha kufanya mambo yanayoweza kupelekea kupata au kuambukizwa magonjwa hayo kwani matibabu yake ni gharama, kinga ni bora kuliko tiba.
Kwa upande wake Juliana Ntukey
Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ameeleza kuwa watumishi wanasisitizwa kutambua kuwa suala la afya dhaifu huathiri uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi pia humuathiri mtumishi binafsi hivyo watumishi wenyewe wanawajibika katika kujali afya zao kama ilivyofafanuliwa katika kanuni 105(2) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003.
“Kila mtumishi wa Umma anawajibika kuchukua tahadhari dhidi ya vichocheo vinavyoweza kuathiri afya yake” alisisitiza Juliana.
Nae Ulimbakisya Masomeru Meneja wa Sehemu ya Utawala TALIRI ameshukuru kwa mafunzo hayo muhimu kwani afya bora za watumishi hupelekea kuwepo kwa matokeo bora ya uwajibikaji wa watumishi kwenye Taasisi.