TALIRI YAHAMASISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ZA KISASA ZA MIFUGO, NANENANE
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imeanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu teknolojia mbalimbali za kisasa za mifugo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha matumizi ya teknolojia zinazoongeza tija na kuimarisha sekta ya mifugo nchini.
Wananchi mbalimbali wamejitokeza kutembelea banda la TALIRI kwa lengo la kujifunza teknolojia na bunifu mbalimbali zinazotokana na tafiti za kisayansi zinazolenga kuongeza uzalishaji, kuboresha afya ya mifugo na kuinua kipato cha wafugaji.
Katika banda hilo, wataalamu wa TALIRI wanatoa elimu kuhusu mbari bora za mifugo ikiwemo ng’ombe, mbuzi na kuku, teknolojia za uzalishaji na uhifadhi wa malisho, utengenezaji za vyakula ziada vya mifugo, pamoja na matumizi ya teknolojia mbalimbali zinazowawezesha wafugaji kuongeza uzalishaji kwa gharama nafuu na kwa ufanisi zaidi.
Aidha, wananchi wanapata fursa ya kujionea matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa na TALIRI, bunifu za kisasa pamoja na teknolojia zinazosaidia kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo na kuchochea maendeleo endelevu ya ufugaji nchini.
Akizungumza katika banda la TALIRI, Mtaalamu wa Taasisi hiyo, Bi. Grace Ayo, amesema TALIRI itaendelea kufanya tafiti zenye kuzingatia mahitaji halisi ya wafugaji na kusambaza teknolojia zinazowawezesha kuongeza tija na ushindani katika shughuli za uzalishaji wa mifugo.
“Lengo letu ni kuhakikisha matokeo ya tafiti yanawafikia wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo kwa wakati, ili yaweze kutumika kuongeza uzalishaji, kuboresha kipato na kuchangia maendeleo ya sekta ya mifugo na uchumi wa Taifa,” amesema Bi. Ayo.
Bi. Ayo ameeleza kuwa ushiriki wa TALIRI katika Maonesho hayo no kutoa fursa kwa wananchi kukutana moja kwa moja na wataalamu wa taasisi hiyo, kupata ushauri wa kitaalamu na kujifunza teknolojia zinazoweza kutumika katika mazingira yao ya ufugaji.
