TEKNOLOJIA YA UHIMILISHAJI WA KUKU WA KIENYEJI YAVUTIA WAFUGAJI BANDA LA TALIRI
Wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo wanaoendelea kutembelea banda la Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya John Samwel Malecela, jijini Dodoma, wanaendelea kunufaika na elimu ya kitaalamu, ushauri pamoja na teknolojia mbalimbali za kisasa zilizobuniwa na Taasisi hiyo kwa lengo la kuongeza tija, uzalishaji na kipato cha wafugaji.
Miongoni mwa teknolojia zinazovutia wananchi ni pamoja na teknolojia ya uhimilishaji wa kuku wa kienyeji, ambayo imeelezwa kuwa suluhisho muhimu la kuongeza uzalishaji wa mayai na vifaranga kwa kutumia mbegu bora za jogoo, huku ikipunguza gharama za uzalishaji na kuboresha ubora wa mifugo.
Akitoa elimu kwa wageni wanaotembelea banda la TALIRI, mtaalamu wa Taasisi hiyo, Dkt. Ngasa Julius, amesema teknolojia ya uhimilishaji wa kuku wa kienyeji humwezesha mfugaji kutumia mbegu za jogoo mmoja kuhimilisha matetea wengi kwa wakati mmoja, hatua inayoongeza ufanisi wa uzalishaji na kurahisisha usimamizi wa mifugo.
Dkt. Ngasa amefafanua kuwa kwa kutumia teknolojia hiyo, mfugaji anaweza kuvuna mbegu kutoka kwa jogoo mmoja na kuhimilisha matetea kati ya 6 hadi 8 na mbegu hizo huweza kukaa hadi dakika 30 kwa uvunaji mmoja wa mbegu katika mazingira ya kawaida.
Kwa mujibu wa Dkt. Ngasa, teknolojia hiyo pia hutoa fursa ya kutumia mbegu za majogoo wenye sifa bora za uzalishaji hata pale wanapokuwa na changamoto za ulemavu wa viungo. Alisema endapo jogoo huyo ana uwezo wa kuzalisha mbegu bora, mbegu hizo zinaweza kuvunwa na kutumika kuhimilisha matetea, hivyo kuhifadhi na kuendeleza sifa bora za kijenetiki katika uzalishaji wa kuku wa kienyeji.
Aidha, Dkt. Ngasa amesema matumizi ya teknolojia ya uhimilishaji huchangia kudhibiti maambukizi ya magonjwa ya kuku kwa kupunguza muingiliano wa kuku bandani, alieleza kuwa hali hiyo hupunguza uwezekano wa kusambaza magonjwa ya kuambukiza, na hivyo kusaidia kupunguza vifo vya kuku pamoja na hasara zinazoweza kuwakumba wafugaji.
