Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
FAO YAPONGEZA TEKNOLOJIA ZA TALIRI KWA KUCHOCHEA MAPINDUZI YA SEKTA YA MIFUGO
10 Aug, 2026
FAO YAPONGEZA TEKNOLOJIA ZA TALIRI KWA KUCHOCHEA MAPINDUZI YA SEKTA YA MIFUGO

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) nchini Tanzania, Dkt. Nyabenyi Tito Tipo, ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa kuendelea kuibua na kuendeleza teknolojia bunifu zinazochangia kuongeza tija katika uzalishaji wa mifugo, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, pamoja na kuongeza kipato cha wafugaji nchini.

Pongezi hizo amezitoa baada ya kutembelea banda la TALIRI katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, jijini Dodoma, ambapo alipata fursa ya kujionea tafiti na teknolojia mbalimbali zinazobuniwa na kuendelezwa na taasisi hiyo kwa lengo la kuleta mageuzi katika sekta ya mifugo.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Dkt. Tipo amesema amevutiwa na teknolojia bora za mifugo zilizozalishwa na TALIRI, akieleza kuwa ni suluhisho muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wafugaji na kuongeza uzalishaji wenye tija.

Dkt. Tipo amesema ubunifu unaofanywa na watafiti wa TALIRI unaonesha uwezo mkubwa wa wataalamu wa Tanzania katika kuzalisha teknolojia zinazoweza kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama, kuboresha lishe ya mifugo, kupunguza gharama za uzalishaji na kuchochea maendeleo endelevu ya sekta ya mifugo.

“FAO itaendelea kushirikiana na TALIRI katika kuhakikisha teknolojia hizi muhimu zinawafikia wafugaji wengi zaidi nchini ili ziweze kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na lishe, pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa,” amesema Dkt. Tipo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Vitus Komba, amesema taasisi hiyo itaendelea kuwekeza katika tafiti na ubunifu wa teknolojia zinazolenga kuboresha sekta ya mifugo, ikiwemo uboreshaji wa mbari za mifugo, uzalishaji wa malisho na mbegu bora za malisho na uendelezaji wa vyakula vya ziada vya mifugo.

Prof. Komba amesema teknolojia hizo zina mchango mkubwa katika kuongeza tija ya uzalishaji, kuboresha maisha ya wafugaji, kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kuunga mkono juhudi za Serikali za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.