Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
BALOZI MWADINI AITAKA TALIRI KUSAMBAZA TEKNOLOJIA KWA WAFUGAJI
12 Aug, 2025
BALOZI MWADINI AITAKA TALIRI KUSAMBAZA TEKNOLOJIA KWA WAFUGAJI

Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe. Ali Mwadini ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuhakikisha matokeo ya tafiti zinazofanywa na taasisi hiyo zinawafikia wafugaji ili waweze kufuga kwa tija.

Mhe. Balozi Mwadini amesema hayo tarehe 05/08/2025 alipotembelea banda la TALIRI katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ‘Nanenane’ yanayoendelea ndani ya viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

“Nimefurahi sana na kufarijika na tafiti zinazofanywa na Taasisi hii hasa tafiti za malisho nimeona aina nyingi za mbegu za malisho zilizofanyiwa utafiti na kupatiwa ithibati, kazi hii kubwa inayofanyika inatakiwa ijulikane na iwafikie wafugaji kote nchini” alisema Mhe. Balozi Mwadini.

Pamoja na hayo Mhe. Mwadini ameipongeza taasisi hiyo kwa kuzalisha teknolojia bora za mifugo na ametoa wito kwa wafugaji kuitumia taasisi hiyo vizuri ili kuongeza tija kwenye shughuli zao za ufugaji.

Kwa upande wake Meneja wa Sehemu ya Uhaulishaji wa Teknolojia Bw. Gilbert Msuta ameeleza kuwa katika kufikisha teknolojia bora za mifugo zilizozalishwa na Taasisi hiyo kwa wafugaji TALIRI imekuwa ikifanya program za kuwatembelea wafugaji kwenye maeneo hayo ‘outreach program’ semina na maonesho mbalimbali na vyombo vya habari kwa ajili ya kutoa elimu kwa wafugaji lakini pia inatoa fursa kwa wafugaji kote nchini kutembelea ofisi za TALIRI zilizopo kwenye kanda zote nchini ili kujipatia elimu juu ufugaji bora.

Msuta ameongeza kuwa mbali na teknolojia hizo wafugaji na wadau mbalimbali wanaotembelea banda hilo wanapata fursa ya kujionea kifaa maalumu kilichotengenezwa kwa ajili ya kuwezesha matumizi rahisi ya kupima uzito, kuwezesha utoaji wa huduma za matibabu kwa mifugo pamoja na kutunza taarifa muhimu za mifugo.

Teknolojia bora za mifugo zilizozalishwa na taasisi hiyo ni pamoja na teknolojia ya malisho na mbegu za malisho, mbari za mifugo pamoja na vyakula vya mifugo.

#taliriutafitikwamaendeleo