Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
WATAFITI TALIRI WAFANYA ZIARA YA KUTEMBELEA WAFUGAJI
23 Sep, 2025
WATAFITI TALIRI WAFANYA ZIARA YA KUTEMBELEA WAFUGAJI

Watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) wakiongozwa na Meneja wa Sehemu ya Uhaulishaji wa Teknolojia za Mifugo wa Taasisi hiyo Bw. Gilbert Msuta wakiongozana na Afisa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Fadhili Chamwazi wamefanya ziara ya kutembelea kikundi cha wafugaji Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Kata Segala kwa lengo la kuwapatia ushauri wafugaji hao juu ya namna bora ya kuendeleza ufugaji wenye tija.

Kikundi hicho kiitwacho ‘Mallya Goat Association’ kwa sasa kinajishughulisha na ufugaji wa mbuzi aina ya Mallya pekee ikiwa ni moja ya teknolojia bora za mifugo zilizozalishwa na TALIRI.

Akiongea wakati wa kutoa elimu ya ufugaji bora kwa lengo la kuongeza ustawi wa mifugo Meneja Msuta amewashauri wafugaji hao kupanda malisho bora ya mifugo ili kuwa na uhakika wa chakula cha mifugo hasa kipindi cha kiangazi na kwamba Taasisi ipo tayari kuwapatia mbegu za malisho aina ya CENCHRUS CIRIALIS kwa ajili ya kuotesha msimu wa mvua.

Pamoja na hayo Meneja Msuta amewataka wafugaji hao kuhakikisha wanatambua mbuzi wote kwa kuwawekea hereni na kusimamia vizazi vya mbuzi kwa kuhakikisha wanabadilisha madume ya mbuzi hao kila mara inapohitajika kuepuka kuzaliana ndani ya ukoo ili kuongeza uzalishaji na ufanisi.

Aidha, wafugaji hao wametakiwa kuhakikisha wanazingatia utoaji wa chanjo na matibabu ya mbuzi kwa ujumla ili kuendelea kuwa na mbuzi bora, pia wamewashauri kuboresha miundombinu ya josho na mabirika ya kunyweshea mbuzi maji kwa ustawi wa mifugo yao.

Nae, Mwenyekiti wa Kikundi hicho Bw. Said Kajeku akiongea kwa niaba ya wanakikundi wengine amesema wamefarijika sana kwa kupata elimu hiyo yenye tija na wanaishukuru sana TALIRI kwa kuwaahidi kuwapatia maduke ya mbuzi pamoja na mbegu za malisho na kueleza kuwa wataanza kutenga eneo la ekari mbili kwa ajili ya kupanda malisho hayo.