Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI YASAJILI AINA TANO YA MBEGU ZA MALISHO
10 Oct, 2024
TALIRI YASAJILI AINA TANO YA MBEGU ZA MALISHO

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imefanikiwa kukamilisha utafiti na usajili wa aina tano za mbegu za malisho ya mifugo zitakazosaidia kurahisisha upatikanaji wa malisho ya mifugo jambo ambalo litasaidia kumaliza migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Mbegu hizo ni pamoja na _Cenchrus ciliaris_ (TALIRICENCH 1), _Medicago sativa _(TALIRIALFA 1), _Desmodium intortum_ (TALIRIDESMO 1), _Macroptilium atropurpureum_ (TALIRIMACRO 1) na _Chloris gayana_ (TALIRICHLO 1) ambapo mkakati wa Taasisi hiyo ni kuzizalisha kwa wingi na kuzisambaza kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.

Akizungumza leo tarehe 07/08/2024 kwenye Maonesho ya 31 ya Kilimo ya Kimataifa (Nanenane) viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick Vitus Komba amesema kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ya uzalishaji wa mbegu chini ya kifungu cha 21 cha sheria ya mbegu Na. 18 ya mwaka 2003 na marekebisho yake ya mwaka 2014 Serikali imeidhinisha matumizi ya mbegu hizo.

Aidha, Prof. Komba ameeleza kuwa mara baada ya kukamilisha usajili huo mkakati wa taasisi hiyo ni kuhakikisha mbegu hizo zinapatikana kwenye maduka ya pembejeo za kilimo kama ilivyo kwa mbegu za mazao mbalimbali.

Kwa upande wake Mtafiti wa taasisi hiyo Ndg. Jovith Alphonce Kajuna ameeleza kuwa utafiti wa mbegu hizo umeonesha mbegu hizo zina ubora wa kutosha na zitakuwa ni suluhisho la upatikanaji wa malisho ya mifugo na hivyo kuwezesha ufugaji wenye tija.

Itakumbukwa kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi mara kadhaa imekuwa ikiwasisitiza wafugaji kuwa na mashamba ya malisho ili kuwa na uhakika wa chakula kwa mifugo yao hivyo kukamilika kwa utafiti huo na usajili itawezesha lengo hilo kufikiwa.