Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI YASAJILI AINA TANO YA MBEGU ZA MALISHO
19 Jul, 2024
TALIRI YASAJILI AINA TANO YA MBEGU ZA MALISHO

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imefanikiwa kukamilisha utafiti na usajili wa aina tano za mbegu za malisho, ikiwemo mbegu aina ya _Cenchrus ciliaris_ (TALIRICENCH 1), _Medicago sativa_ (TALIRIALFA 1), _Desmodium intortum_ (TALIRIDESMO 1), _Macroptilium atropurpureum_ (TALIRIMACRO 1) na Chloris _gayana_ (TALIRICHLO 1) mbegu hizo zitapatikana madukani na wafugaji watazitumia kuzalisha malisho kwa ajili mifugo yao.

Hayo yameelezwa leo tarehe 13/07/2024 na Mkurugenzi wa Utafiti wa Mifugo wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Dkt. Andrew Chota kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ‘Sabasaba’ yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

Dkt. Chota ameendelea kueleza kuwa jitihada za kutekeleza agizo hilo ni kwenda sambamba na maono ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuona mwelekeo mpya wa ufugaji nchini na msukumo wa Mhe. Abdallah Hamis Ulega (Mb.) Waziri wa Mifugo na Uvuvi na watendaji wa Wizara wa kuona maono na maelekezo hayo ya Mhe. Rais yanafanyiwa kazi.

“Itakumbukwa kuwa Mhe. Ulega mara kadhaa amewasisitiza wafugaji kuwa na mashamba ya malisho ili kuwa na uhakika wa chakula kwa mifugo yao” amesema Chota.

Aidha, Dkt. Chota ameeleza kuwa baada ya mbegu hizo kufanyiwa utafiti na takwimu za ubora kuwasilishwa kwenye Taasisi Rasmi ya Uthibitisho wa Mbegu ‘Tanzania Official Seed CertificationI nstitute - TOSCI’ ilifanyia kazi na Kamati ya Taifa ya Kupitisha Aina Mpya za Mbegu ‘The National Variety Release Committee - NVRC’ ilipendekeza kwa Kamati ya Taifa ya Mbegu ‘National Seed Committee - NSC’ kuwa mbegu hizo sijaliwe.

“TALIRI na Umma umejulishwa rasmi kuwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ya uzalishaji wa mbegu na chini ya kifungu cha 21 cha sheria ya mbegu Na. 18 ya mwaka 2003 na marekebisho yake ya mwaka 2014 Mhe. Hussein M. Bashe (Mb.) Waziri wa Kilimo, ameidhinisha matumizi ya mbegu hizo tano za malisho” amesema Dkt. Chota.

Akihitimisha mazungumzo hayo Dkt. Chota ametoa wito kwa wafugaji wote kuwekeza kwenye malisho kama hatua muhimu ya kuongeza tija kwenye uzalishaji.