TALIRI YAJIVUNIA MAFANIKIO LUKUKI SIKU 100 ZA UONGOZI WA RAIS SAMIS
You said:
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) inajivunia mafanikio mbalimbali ndani ya siku 100 za mwanzo za kipindi cha pili cha Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Akiongelea mafanikio hayo Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Erick Komba amesema ndani ya siku hizo Taasisi imefanikiwa kusambaza teknolojia bora za mifugo 14,825 zikiwemo mbari za mifugo, malisho na mbegu za malisho kwa wafugaji 133 katika mikoa mbalimbali nchini. Vilevile Prof. Komba ameeleza kuwa Taasisi imefanikiwa kutoa mafunzo juu ya upandaji, uhifadhi na utunzaji wa malisho, urejeshaji wa uoto wa asili, uzalishaji wa mbari bora za mifugo na utayarishaji wa lishe ya mifugo kwa wafugaji 863 katika mikoa mbalimbali nchini. Prof. Komba ameongeza kuwa taasisi imefanikiwa kupata watumishi wa ajira mpya 36 kati yao 16 ni Watafiti Wasaidizi na 20 ni Maafisa Shamba. “Ajira hizi zimeimarisha uwezo wa Taasisi yetu katika kufanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto za uzalishaji, magonjwa ya mifugo na athari za mabadiliko ya tabianchi, huku Maafisa Shamba wakihakikisha matokeo ya tafiti yanawafikia wafugaji” amesema Prof. Komba. Pamoja na hayo Prof. Komba amesema Taasisi inaendelea kushirikiana na wafugaji mbalimbali ambao wamekuwa wakitumika kama mabalozi wa TALIRI katika kusambaza teknolojia bora za mifugo zilizozalishwa na TALIRI kwa wafugaji wengine kitendo ambacho kimewezesha teknolojia hizo kufikia wafugaji wengi zaidi. Akiongelea matarajio ya Taasisi Prof. Komba amesema katika kipindi hiki cha pili cha Awamu ya Sita, TALIRI itaendelea kufanya tafiti zenye kuleta suluhisho la changamoto za ufugaji na kuhakikisha elimu ya ufugaji bora sambamba na teknolojia bora za mifugo zinawafikia wafugaji kote nchini, lengo ikiwa ni kubadilisha sekta ya mifugo kutoka ufugaji wa asili kwenda ufugaji wa kisasa, kibiashara na wenye tija. Katika siku hizo 100 Serikali imeendelea kuonesha dhamira thabiti ya kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Mifugo kwa vitendo sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inayolenga kujenga uchumi wa kati ambao unategemea uzalishaji wenye tija
