TALIRI YATOA ELIMU KWA WAGENI WA KIMATAIFA KUHUSU TEKNOLOJIA BORA ZA UFUGAJI
Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Bw. Ezekiel Maro, akitoa elimu kwa wageni kutoka nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Namibia, Angola, Malawi, Botswana, Zimbabwe na Zambia, waliotembelea Tanzania kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu kilimo endelevu cha misitu na ufugaji wa nyuki.
Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mandhari ya Ardhi katika Misitu ya Miombo Kavu Tanzania (DSL-IP).
Katika ziara hiyo, wageni hao pia walipata fursa ya kujifunza teknolojia mbalimbali zilizofanyiwa utafiti na kuzalishwa na TALIRI, zikiwemo mbari bora za mifugo, aina bora za malisho na mbegu zake, pamoja na teknolojia za kuboresha lishe ya mifugo.
Kupitia ziara hiyo, TALIRI inaendelea kuonesha mchango wa utafiti katika kutoa suluhisho endelevu kwa maendeleo ya sekta ya mifugo na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kupitia kubadilishana maarifa na uzoefu.
Kupitia jukumu lake katika mradi huo, TALIRI inaendelea kuchangia upatikanaji wa teknolojia na maarifa ya kisayansi yatakayosaidia kuendeleza mifumo endelevu ya uzalishaji wa mifugo, kuboresha usimamizi wa rasilimali za malisho na kuimarisha ustahimilivu wa jamii zinazotegemea rasilimali za misitu ya Miombo.
