TALIRI YAANGAZIA NAFASI YA NYUKI KATIKA UHIFADHI WA MISITU YA MIOMBO
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imewasilisha matokeo ya tafiti na mchango wake katika kuendeleza mifumo endelevu ya uzalishaji wa mifugo na usimamizi wa rasilimali za malisho kwa wageni kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo Namibia, Angola, Malawi, Botswana, Zimbabwe na Zambia waliotembelea Tanzania kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu juu ya kilimo endelevu cha misitu na ufugaji wa nyuki ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mandhari ya Ardhi katika Misitu ya Miombo Kavu Tanzania.
Katika wasilisho hilo lililowasilishwa katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo (MAT) kilichopo Tumbi Mkoani Tabora, Mkurugenzi wa Utafiti wa taasisi hiyo Dkt. Andrew Chota aliangazia uhusiano uliopo kati ya ufugaji wa mifugo, ufugaji nyuki, kilimo na uhifadhi wa mazingira, akieleza namna shughuli hizo zinavyoweza kuunganishwa katika matumizi endelevu ya rasilimali za ardhi ili kuongeza uzalishaji na kulinda mifumo ya ikolojia.
Aidha, wasilisho lilieleza matokeo ya uchunguzi wa kisayansi kuhusu ubora wa asali inayozalishwa katika misitu ya Miombo, ikiwemo sifa zake za lishe, uwezo wa kupambana na baadhi ya bakteria na viambato vya kupambana na madhara ya seli huru mwilini. Vilevile, changamoto zinazoathiri afya ya nyuki, kama vile uharibifu wa misitu, moto, matumizi ya viuatilifu, mabadiliko ya tabianchi na magonjwa ya nyuki, zilijadiliwa pamoja na hatua za kuzidhibiti.
Katika eneo la ufugaji wa mifugo, TALIRI ilisisitiza umuhimu wa kusimamia rasilimali za malisho, matumizi salama ya dawa za mifugo na upangaji bora wa matumizi ya ardhi ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kati ya shughuli za ufugaji wa mifugo na ufugaji nyuki. Mambo hayo yalielezwa kwa kuzingatia mkabala wa Afya Moja (One Health), unaounganisha afya ya binadamu, wanyama na mazingira.
Vilevile, washiriki walipata maelezo kuhusu fursa za kuongeza thamani ya mazao ya nyuki, kuimarisha ubora wa asali na kukidhi viwango vinavyohitajika katika masoko ya kimataifa, hatua zinazoweza kuongeza kipato cha wafugaji na kuchochea maendeleo ya uchumi wa vijijini.
Mradi wa DSL-IP unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani (Global Environment Facility – GEF) kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Food and Agriculture Organization – FAO), ukiwa na lengo la kukuza usimamizi jumuishi wa mandhari ya ardhi, kurejesha maeneo yaliyoharibika na kuhifadhi bioanuwai katika misitu ya Miombo.
Kupitia jukumu lake katika mradi huo, TALIRI inaendelea kuchangia upatikanaji wa teknolojia na maarifa ya kisayansi yatakayosaidia kuendeleza mifumo endelevu ya uzalishaji wa mifugo, kuboresha usimamizi wa rasilimali za malisho na kuimarisha ustahimilivu wa jamii zinazotegemea rasilimali za misitu ya Miombo.
