TALIRI YATAKIWA KUONGEZA NGUVU KWENYE TAFITI ZENYE KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Fabian Madele ameielekeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuongeza nguvu katika kufanya tafiti zinazolenga kutatua changamoto halisi za wafugaji ili kuchochea maendeleo ya sekta ya mifugo na kuongeza tija nchini.
Dkt. Madele ametoa maelekezo hayo leo Mei 20, 2026 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kituo cha TALIRI Kanda ya Mashariki, ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Katika ziara hiyo, Dkt. Madele amesema tafiti zinazofanywa na TALIRI zinapaswa kuendana na mahitaji ya sasa ya wafugaji pamoja na mabadiliko ya sekta ya mifugo, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia tafiti hizo kama nyenzo ya kuongeza uzalishaji, kuboresha afya za mifugo na kuinua uchumi wa wafugaji.
Aidha, ameiagiza taasisi hiyo kuongeza kasi ya usambazaji wa teknolojia bora za mifugo zilizoibuliwa na watafiti wake, ikiwemo uendelezaji wa mbari bora za mifugo, uzalishaji wa malisho na mbegu zake, pamoja na teknolojia za vyakula vya ziada kwa mifugo ili kusaidia kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa lishe bora kwa mifugo hususani kipindi cha ukame.
Dkt. Madele pia ameihimiza TALIRI kupanua wigo wa tafiti zake kwa kujielekeza katika ufugaji wa wanyama wengine wenye fursa kubwa kiuchumi ambao bado hawajapewa kipaumbele cha kutosha nchini, akiwemo sungura na kwale, hatua aliyosema inaweza kusaidia kufungua masoko mapya na kuongeza ajira pamoja na kipato kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Komba, amesema taasisi hiyo itaendelea kuimarisha tafiti zenye matokeo chanya kwa wafugaji na kuhakikisha teknolojia zinazozalishwa zinawafikia wananchi kwa wakati ili kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika Pato la Taifa.
Prof. Komba amesema TALIRI imejipanga kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo katika kubuni na kusambaza teknolojia zinazolenga kuongeza uzalishaji, kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usalama wa chakula na lishe nchini.
