Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI YAHAMASISHA WANANCHI KUTEMBELEA BANDA LAKE WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2026
18 Jun, 2026
TALIRI YAHAMASISHA WANANCHI KUTEMBELEA BANDA LAKE WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2026

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) imewakaribisha wafugaji, wadau wa sekta ya mifugo na wananchi kwa ujumla kutembelea banda la taasisi hiyo katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, kwa lengo la kupata elimu na huduma mbalimbali za kiutumishi na utafiti wa mifugo. Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Profesa Erick Komba, amesema taasisi hiyo imejipanga kutoa elimu kuhusu masuala ya kiutumishi ikiwemo sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya utumishi wa Umma kwa watumishi na wadau wanaotembelea banda hilo. Prof. Komba amesema kuwa pamoja na elimu ya kiutumishi, TALIRI pia inatoa elimu kuhusu shughuli za utafiti wa mifugo, zikiwemo teknolojia za malisho na mbegu bora za malisho, mbari bora za mifugo, afya ya mifugo pamoja na mbinu mbalimbali za ufugaji wenye tija. Ameeleza kuwa maonesho hayo yanatoa fursa kwa wafugaji na wadau kupata taarifa sahihi kuhusu teknolojia zilizobuniwa na TALIRI pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu na majibu ya papo kwa papo juu ya changamoto wanazokutana nazo katika shughuli za ufugaji. Aidha, Prof. Komba amesema TALIRI inaendelea kufanya tafiti na kuendeleza ubunifu unaolenga kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mifugo nchini, huku akisisitiza kuwa teknolojia hizo zimebuniwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya wafugaji wa Tanzania. “Teknolojia hizi zina mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji, kuboresha afya ya mifugo, kuhifadhi mazingira na kukuza uchumi wa wafugaji pamoja na taifa kwa ujumla,” amesema Prof. Komba. Ameongeza kuwa ushiriki wa TALIRI katika Maadhimisho hayo ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo za kuhakikisha matokeo ya tafiti na ubunifu wake yanawafikia wananchi moja kwa moja na kutumika katika kuboresha maisha ya wafugaji na kuendeleza sekta ya mifugo nchini.