KATIBU MKUU UTUMISHI AIPONGEZA TALIRI KWA UBUNIFU WA TEKNOLOJIA ZA MIFUGO Katibu
Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa juhudi zake za kufanya utafiti, ubunifu na kuendeleza teknolojia mbalimbali zinazochangia maendeleo ya sekta ya mifugo nchini. Pongezi hizo amezitoa leo Juni 16, 2026 alipotembelea banda la TALIRI katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma. Katibu mkuu huyo alipata fursa ya kujionea teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na TALIRI kwa lengo la kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya mifugo. Bw. Mkomi alisema kuwa ubunifu unaofanywa na TALIRI una mchango mkubwa katika kusaidia juhudi za Serikali za kuleta mageuzi katika sekta ya mifugo na kuhakikisha wafugaji wanatumia teknolojia zinazowawezesha kuzalisha kwa tija na ushindani zaidi. Kwa upande wake Bw. John Diyu Mtafiti kutoka TALIRI amesema katika maonesho hayo wananchi wanapatiwa elimu juu ya teknolojia mbalimbali za kisasa zinazolenga kuboresha uzalishaji wa mifugo, kuimarisha lishe ya mifugo, kuongeza uzalishaji wa maziwa na nyama pamoja na kuboresha kipato cha wafugaji nchini. Aidha, Bw. Diyu amesema TALIRI itaendelea kufanya tafiti na kuibua teknolojia bunifu zitakazosaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya mifugo huku ikichangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia ongezeko la uzalishaji na thamani ya mazao ya mifugo. Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026 yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu,” yakilenga kuhamasisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi kupitia uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali
