TALIRI,ILIRI NA WIZARA YA MIFUGO KUUNGANISHA MIFUMO YA TAKWIMU NA UTAMBUZI WA MIFUGO NCHINI
Ikiwa ni muendelezo wa utekelezaji wa shughuli za Mradi wa Uboreshaji wa Vinasaba vya Ng’ombe wa Maziwa Katika Ukanda wa Kitropiki (TDGG) ambao zamani ulitambulika kama Mradi wa Uboreshaji wa Vinasaba vya Ng’ombe wa Maziwa Afrika na Asia (AADGG) Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo (ILRI) ambao ni watekelezaji wa mradi huo wamekutana na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili kujadili namna ya kuunganisha Mfumo wa Kukusanyia taarifa za Maziwa ulioanzishwa na mradi huo na Mfumo wa Utambuzi wa Mifugo na Chanjo wa Wizara hiyo.
Akielezea suala hilo Mratibu wa Mradi huo Dkt.Eliamoni Lyatuu kutoka ILRI amesema mradi umelenga kuona wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa wanapata mbegu bora zaidi za ng’ombe wa maziwa, huduma za uzalishaji na elimu, pamoja na huduma muhimu za pembejeo zinazowezesha shughuli zao za ufugaji kuwa za tija na ushindani.
Dkt. Lyatuu ameendelea kueleza kuwa kupitia mifumo hiyo taarifa muhimu za ufugaji zitakusanywa na kutunza kwa ufanisi na hivyo kuwezesha kusimamia vyema uzalishaji wa maziwa, uzito wa mifugo, ufanisi katika uzalishaji wa mifugo hiyo, uwezo wa kuingia joto, uvumilivu wa magonjwa, uendelevu wa maziwa kwenye kizazi, kupunguza uzalishaji wa hewa ya methane, viwango vya kuishi kwa mifugo husika na udhibiti wa viashiria vya uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Bw. Gilbert Msuta ambaye pia ni Mtafiti Mwandamizi wa Mradi huo kutoka TALIRI amesema mbali na mifumo hiyo mradi kwa kushirikiana na Wizara umepanga kuanzisha Mfumo wa Kitaifa wa Tathmini ya Vinasaba na Uthibitisho wa Madume bora kwa Ajili ya Uzalishaji wa Ng’ombe wa Maziwa nchini Tanzania, kwani wafugaji wengi wa ng’ombe wa maziwa nchini wanakumbana na changamoto ya kupata mbari bora za mifugo.
Bwana Msuta ameendelea kueleza kuwa tathmini ya vinasaba vya mifugo katika mifumo ya ufugaji wa kaya itasaidia kuharakisha utambuzi na matumizi ya mifugo yenye uzalishaji bora lakini pia mfumo wa uthibitishaji utaimarisha soko la mifugo hai ndani na nje ya nchi na kuhakikisha vinavyotolewa ni vya kuaminika na vinaendelea kudumishwa.
