Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
TALIRI YAENDELEZA TAFITI ZA MIFUGO
19 Jul, 2024
TALIRI YAENDELEZA TAFITI ZA MIFUGO

Katika kuhakikisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) inatekeleza jukumu la kubaini, kutathmini na kusambaza teknolijia bora za mifugo taasisi hiyo imeendelea kufanya tafiti mbalimbali za mifugo ikiwemo utafiti wa vyakula vya mifugo, utafiti wa malisho yaliyoboreshwa, utafiti wa magonjwa ya mifugo, utafiti wa tabia za mifugo pamoja na kutumia virutubisho vya asili kwa mifugo.

Akiongelea utafiti wa malisho yaliyoboreshwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Prof. Erick Komba ameeleza kuwa lengo la utafiti huo ni kumuwezesha mfugaji kuwa na uhakika wa chakula bora cha mifugo na kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Prof. Komba ameeleza kuwa kwa kutumia malisho yaliyoboreshwa mfugaji anaweza kutumia heka 2.5 kwa mwaka kumtunza ng’ombe mmoja wakati kwa kutumia malisho ya asili ambayo hayapatikani katika maeneo mengi mfugaji anaweza kutumia zaidi ya heka 10 kutunza ng’ombe mmoja kwa mwaka.

Sambamba na hayo Prof. Komba ameeleza kuwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na kampuni ya ‘Afrint Bio Solution Limited’ ya Nchi ya Indonesia inayojishughulisha na utengenezaji wa virutubisho vya asili kwa ajili ya mifugo, samaki na mazao yakiwemo malisho ili kuhakikisha utafiti wa mifugo kwa kutumia virutubisho asilia unafanyika kama ambavyo sheria inaielekeza taasisi hiyo kufanya hivyo.

“Virutubisho vya kampuni hiyo vina mchanganyiko wa madini mbalimbali na virutubisho vingine ambavyo mnyama akila atatengeneza uwiano mzuri wa wadudu wa tumboni ambao wanasaidia kukuza kinga ya mwili, lakini pia kuwezesha matumizi mazuri ya chakula mwilini mwa mnyama, ukuaji mzuri na faida zingine” aliongeza Prof. Komba.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kampuni ya ‘Afrint Bio Solution Limited’ Bw. Emmanuel Paluku amesema lengo la kampuni hiyo kutengeneza bidhaa hizo za virutubisho vya asili ni kupunguza matumizi ya kemikali zinazopatikana kwenye viuatilifu vya mifugo, kilimo na uvuvi ambavyo vinatajwa kusababisha madhara kwa watumiaji.