TALIRI YAINGIA USHIRIKIANO NA TAASISI YA CHINA KUIMARISHA TAFITI ZA MIFUGO NCHINI
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) inatarajia kuingia ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo ya Lanzhou, Chuo cha Sayansi ya Kilimo cha China (LVRI - CAAS) katika kuendeleza tafiti mbalimbali za mifugo kwa lengo la kuboresha tija katika sekta hiyo nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Mhina Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, amesema ushirikiano huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa sekta ya mifugo kwa kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafugaji.
Akiwasilisha taarifa ya jinsi China imefanikiwa kudhibiti magonjwa mbalimbali ya mifugo ikiwemo ugonjwa wa miguu wa mdomo kwa mifugo Prof. Liu Zhijie amesema nchi hiyo imepiga hatua kubwa katika kudhibiti ugonjwa huo.
Ameongeza kuwa China iko tayari kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha changamoto mbalimbali za mifugo katika maeneo ya afya na uzalishaji zinatatuliwa.
Aidha, Dkt. Liu alieleza kuwa kuenea kwa magonjwa ya mifugo kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na mfumo wa ufugaji wa kuhama hama pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Komba, amesema taasisi hiyo itashirikiana na LVRI - CAAS katika maeneo mbalimbali ikiwemo tafiti za magonjwa ya mifugo, uzalishaji pamoja na kuwajengea uwezo watafiti na kukuza vipaji kwa watafiti vijana.
