TALIRI WAASWA KUTOSHIRIKI VITENDO VYA RUSHWA
Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Mpwapwa Maura Mntambo ametoa wito kwa watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Kati kituo cha Mpwapwa kutoshiriki vitendo vya rushwa kwani hatua za kisheria zitachukuliwa endapo mtumishi atabainika kushiriki vitendo hivyo.
Wito huo umetolewa leo tarehe 20/11/2024 alipokuwa akiongea na watumishi wa Taasisi hiyo juu ya masuala ya rushwa mahali pa kazi kwa lengo la kuwawezesha watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu.
Maura ameendelea kueleza kuwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa No 11 ya mwaka 2007 imetaja matendo ambayo mtumishi akiyafanya atakuwa ameshiriki vitendo vya rushwa ikiwemo rushwa ya mikataba, minada, ajira, vitendo vya kutoa na kupokea hongo, matumizi mabaya ya nyaraka kwa ajili ya kumdanganya mwajiri, matumizi mabaya ya madaraka, kujilimbikizia mali, ubadhilifu na ufujaji wa fedha za Serikali, kula njama, kumsaidia mtu kutenda kosa la rushwa na kujifanya kuwa Afisa TAKUKURU.
Sambamba na hayo Maura ameeleza kuwa kila mtumishi anapaswa kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwa kutoa huduma bora, kuwa na utii kwa Serikali, bidiii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa Umma, na kuheshimu sheria lakini pia Viongozi wanapaswa kutumia vizuri madaraka na kufanya ushirikishwaji juu ya masuala mbalimbali ya taasisi kwa watumishi.
“Matokeo ya rushwa hupelekea kukosekana kwa haki kwa anaestahili, kuisababishia Serikali hasara na jamii kwa ujumla, miradi isiyokuwa na ubora unaotakiwa, ununuzi wa vifaa hewa au visivyo na viwango na kuwepo kwa matabaka na chuki miongoni mwa watumishi” aliongeza Maura.
Kwa upande wake Ulimbakisya Masomeru Meneja wa Sehemu ya Utawala wa TALIRI Makao Makuu amempongeza Afisa huyo kwa mafunzo hayo ambayo yataenda kuongeza tija ya uwajibikaji unaostahili kwa watumishi hao na kuwataka kuzingatia yaliyofundishwa kwa kuendelea kuwa waadilifu ili kuepuka kuingia kwenye ushawishi wa vitendo vya rushwa mahali pa kazi kwani hukumu ya aliyethibitika kutenda vitendo hivyo adhabu yake yaweza kuwa kifungo, faini, kufirisiwa, kuachishwa kazi au vyote kwa pamoja.