WANAFUNZI KUTOKA CHUO CHA BORIGARAM WATEMBELEA TALIRI

Wanafunzi kutoka chuo cha Borigaram Agriculture Technical College kilichopo Dar es salaam wametembelea banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es salaam kwa lengo la kujifunza teknolojia mbalimbali za mifugo zilizoibuliwa na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI)
Akiongelea teknolojia za malisho Bw. Ezekiel Maro Afisa Mifugo wa Taasisi hiyo amesema ili kufanya ufugaji wenye tija ni vizuri kutenga eneo la malisho ya mifugo kwa lengo la kuwa na uhakika wa chakula cha mifugo lakini pia kupunguza migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi hususani wakulima pale ambapo mifugo itaingia kwenye mashamba ya wakulima.
Maro ameeleza kuwa TALIRI imependekeza malisho ya aina mbalimbali za nyasi zinazostawi vizuri nchini zikiwemo nyasi aina ya Cenchrus ciliaris, Napier, majani tembo lakini pia mikundekunde pamoja na miti malisho aina ya lukina, mlonge na gliciridia.
“Kwa kawaida mifugo inahitaji chakula kiwango cha asilimia 3% ya uzito wa mwili wake ili kumuwezesha kupata nishati stahiki na nguvu za kutosha mwilini” amesema Maro.
Aidha, Maro ameeleza kuwa mbali na nyasi mifugo pia inahitaji vyakula vya ziada ikiwemo jiwe la madini la kulamba (jiwe lishe) ili kumuwezesha mfugo kupata virutubisho muhimu mwilini.
Akiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzake amesema wamefurahishwa na mafunzo hayo ambayo yataenda kuongeza tija katika masomo yao na hata kuwawezesha kupata hamasa ya kujiajiri wenyewe kwa kufanya ufugaji wenye tija kwa kuwa na uhakika wa malisho ya mifugo.