WADAU WAKUTANA KUJADILI USTAWI WA MNYAMA PUNDA

Wizara ya Mifugo na uvuvi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na wadau wa mnyama punda wakiwemo INADES, ASPA na BROOKE pamoja na wafugaji wa mnyama huyo leo tarehe 16/05/2024 wamekutana katika ukumbi wa hoteli ya Royal Village Dodoma kwa lengo la kujadili ustawi wa mnyama punda nchini.
Akiongea Mkurugenzi wa huduma za ukaguzi na ustawi wa wanyama kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Anette Kitambi ameeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau imejipanga kutoa elimu ya ustawi wa mnyama punda katika shule za msingi, vyuo na wataalamu wa masuala ya mifugo, kufanya utafiti wa kina juu ya mnyama punda pamoja na kuanzisha ufugaji wa punda kwenye mashamba ya wizara.
Dkt. Kitambi ameeleza mipango hiyo kufuatia changamoto zinazomkabili mnyama punda za kutotunzwa vizuri mbali kuwa na umuhimu kwa watumiaji wa mnyama huyo.
Sambamba na hayo Dkt. Kitambi ameeleza kuwa mnamo mwezi oktoba, 2021 Serikali iliweka katazo la kuzuia uchinjaji wa punda na kufunga viwanda vyote vya uchinjaji nchini ili kuhakikisha mnyama punda anaendelea kutunzwa kwani uchinjaji ule ulikuwa unapelekea kupotea kwa mnyama punda nchini.
Kwa upande wake Dkt. Gilbert Msuta Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) amesema taasisi imeendelea kufanya utafiti dhidi ya mnyama punda kwa lengo la kuangalia matumizi ya mnyama huyo, athari za biashara ya kuuza ngozi ya mnyama huyo kwa Taifa pamoja na uhifadhi wa mnyama huyo.
Msuta ameendelea kueleza kuwa TALIRI inaendelea na utafiti kujua ni mzigo wa kiasi gani mnyama punda anamudu kuubeba, uhifadhi wa mbari za punda, kujua namna ya ukuaji wake na mengine yanayomhusu mnyama huyo.
Aidha, Msuta amesema TALIRI itaendelea kutambua mchango wa wafugaji, kutoa elimu kwa jamii juu ustawi wa mnyama punda, kuja na ubunifu wa kusaidia kuongeza ustawi wa mnyama punda, kuja na mpango mkakati wa namna ya kutoa matibabu kwa mnyama punda na kuwa na takwimu sahihi za mnyama huyo ili kuhakikisha ustawi wake unazingatiwa.