Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
SHEMDOE AZINDUA MIUNDOMBINU YA MRADI WA MAZIWA FAIDA TALIRI TANGA
30 May, 2024
SHEMDOE AZINDUA MIUNDOMBINU YA MRADI WA MAZIWA FAIDA TALIRI TANGA

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na uvuvi Mhe. Prof. Riziki Shemdoe akishuhudiwa na Balozi Ireland Tanzania Mhe. Mary O’Neill akizindua miundombinu iliyojengwa kupitia mradi wa maziwa faida unaotekelezwa na kituo cha TALIRI Tanga kwa udhamini wa ubalozi wa Ireland chini ya Taasisi ya Teagacs.

Akiongea katika uzinduzi huo Shemdoe amesema Mradi wa maziwa faida mbali na kuboresha miundombinu mbalimbali lakini pia umekiwezesha kituo hicho kupata vifaa bora vya maabara kwa ajili ya kufanyia tafiti mbalimbali za mifugo na malisho bora.

Shemdoe ameendelea kueleza kuwa lengo la mradi wa maziwa faida ambao umegharimu zaidi ya Bilioni 7 ni kuboresha mnyororo wa thamani wa maziwa kwa wafugaji ambapo kituo cha TALIRI Tanga kimekuwa kikiendelea kutoa mafunzo kwa vitendo juu ya ufugaji wenye tija sambamba na kufanya tafiti mbalimbali za mifugo.

Sambamba na hayo, Shemdoe ametoa wito kwa jamii kuendelea kuzalisha na kutumia maziwa kwa wingi kwani tafiti zinaonesha kuwa watanzania tunapaswa kunywa lita 200 za maziwa kwa mwaka lakini ni kiasi cha lita 50 pekee kinatumika kwa mwaka kwa watanzania wote.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Prof. Erick Komba akimshukuru Rais wa awamu ya sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha mahusiano ya kidemokrasia yaliyopelekea uwepo wa mradi huu muhimu kwa Taifa wenye kuongeza tija kwa wafugaji amesema TALIRI imejipanga vyema kuhakikisha mradi wa maziwa faida unaleta manufaa kwa wafugaji na watumiaji wa mazao ya mifugo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki, TALIRI Tanga Dkt. Zabroni Nziku akielezea mafanikio ya mradi wa maziwa faida amesema Kituo cha TALIRI Tanga kimefanikiwa kutathmini na kujua aina ya malisho bora, kuendelea kufanya tafiti za kupata ng’ombe bora, kuanzisha shamba la mfano la malisho, kuwajengea uwezo watafiti, maafisa ugani na wafugaji ambapo wadau zaidi ya 1000 wamefikiwa na kupatiwa elimu ya ufugaji bora.

Nae balozi wa Ireland Tanzania Mhe. Mary O’Neill ameipongeza TALIRI Tanga kwa namna inavyoendesha mradi huo na kuweza kufikia wadau wengi hususani wafugaji kitendo ambacho kimeleta mabadiliko makubwa kwa wafugaji hao juu ya ufugaji wenye tija.