RAAWU, TALIRI YAFANYA HAFLA YA KUWAKARIBISHA WANACHAMA WAPYA
Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za elimu ya juu, sayansi, teknolojia, ufundi stadi, habari, ushauri na utafiti (RAAWU) Tawi la TALIRI Makao Makuu, wamefanya hafla ya kuwakaribisha wanachama wapya waliojiunga na chama hicho iliyofanyika katika Ukumbi wa Simba Hotel, Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo Katibu wa RAAWU Kanda ya Kati Bi. Staile Kiko, ameeleza kuwa vyama hivi vina msaada mkubwa kwa watumishi kwa kutoa misaada mbalimbali ya kisheria ikiwa mtumishi atahitaji msaada huo muda wowote.
Bi Staile ameongeza kuwa RAAWU ni sauti ya kusemea watumishi juu ya sera mbalimbali na sheria ili kuwatengenezea mazingira mazuri watumishi ya kufanya kazi kipindi chote wawapo kazini hadi ukomo wa ajira utakapofika (kustaafu).
“Mara zote chama kimekuwa mstari wa mbele kusaidia watumishi wanaopata changamoto mbalimbali wanapokuwa kazini tunahakikisha tunashirikiana nao bega kwa bega changamoto zinazowakabili. Chama kina wanasheria ambapo mwanachama yeyote akipata Shauri la mahakamani atasaidiwa bure bila gharama hadi shauri lake litakapotatuliwa ikiwa tu atakuwa chini ya RAAWU.” amesema Bi Staile.
Aidha Bi Staile amewataka wanachama wote hasa wale wanachama wapya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa viongozi wa Tawi la RAAWU TALIRI Makao Makuu unaotarajiwa kufanyika mnamo mwezi Januari ili kupata viongozi watakao wawakilisha watumishi katika mambo mabalimbali. Pia amehimiza watumishi wenye sifa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi hizo.
Nae, Katibu wa Tawi la RAAWU TALIRI Makao Makuu Bw Emmanuel Simule amewataka wanachama kutohisi fedha yao ya michango inakatwa bure kwa kuwa itawasaidia wanachama wengine waliopata changamoto katika maeneo yao ya kazi.
“Vyama vya Wafanyakazi ikiwemo Chama chetu cha RAAWU vinafananishwa na uchangiaji unaofanyika katika mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kwani kwani mwanachama anaweza akachangia kwa muda mrefu bila kuumwa ila michango yake ikasaidia wanachama wengine. Hivyo mtu asipopata tatizo amshukuru MUNGU na mchango wake utamsaidia mtu mwengine.” Amesema Bw. Simule.
#mshikamanodaima
