Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania

TALIRI Logo
PROF. KOMBA AHIMIZA TEKNOLOJIA BUNIFU KUTATUA CHANGAMOTO ZA MIFUGO
27 Apr, 2026
PROF. KOMBA AHIMIZA TEKNOLOJIA BUNIFU KUTATUA CHANGAMOTO ZA MIFUGO

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Prof. Erick Komba, amevitaka vituo vya utafiti vya taasisi hiyo kuimarisha ubunifu wa teknolojia za kisasa za mifugo ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo nchini.

Akizungumza Aprili 22, 2026, wakati wa ziara yake katika Kituo cha Utafiti cha TALIRI Kongwa mkoani Dodoma, Prof. Komba alisema maendeleo ya sekta ya mifugo yanategemea kwa kiasi kikubwa tafiti zenye tija na zinazolenga mahitaji halisi ya wafugaji.

Alisema ni muhimu kwa watafiti kuongeza ufanisi katika uandishi wa maandiko ya kisayansi, utafutaji wa ruzuku, pamoja na uchapishaji wa tafiti ili kuongeza mchango wa taasisi katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

“Tunapaswa kuongeza kasi ya ubunifu na kuhakikisha tafiti zetu zinatoa majibu ya moja kwa moja kwa changamoto za wafugaji,” alisema Prof. Komba.

Aidha, aliwataka watumishi kushiriki kikamilifu katika makongamano ya kitaaluma, kutoa ushauri elekezi na kuimarisha shughuli za uenezi ili tafiti ziwafikie walengwa kwa wakati.

Akizungumzia mikakati ya kufikia malengo ya taasisi, Prof. Komba alisisitiza matumizi ya kanuni ya ukuaji, kuimarisha ushirikiano kazini, kuwa na mipango kazi ya kila mtumishi, kufanya vikao vya mara kwa mara pamoja na kuunda makundi ya kitaaluma katika maeneo ya kipaumbele na kuwajibika ipasavyo.

Katika kikao hicho, watumishi walikumbushwa kuhusu masuala ya utawala pamoja na haki na stahili zao kama watumishi wa Umma.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi Bw. Zacharia Rugora alisisitiza umuhimu wa watumishi kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa Umma katika utekelezaji wa majukumu yao.