WAZIRI MKUU AZINDUA KITUO CHA UFUGAJI MBUZI TALIRI, KONGWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) kuhakikisha elimu ya upandaji wa malisho bora inatolewa kwa wafugaji ili kuepuka migogoro baina ya wakulima na wafugaji pale ambapo mifugo huachiwa na kuingia kwenye mashamba ya wakulima.
Agizo hilo amelitoa leo tarehe 13/05/2024 wakati akizindua na kushuhudia makabidhiano ya kituo atamizi cha ufugaji wa kibiashara kwa vijana katika TALIRI - Kongwa Mkoani Dodoma baina na PASS TRUST kwa kushirikiana na ubalozi wa Dernmark na TALIRI.
Mhe. Majaliwa ameeleza kuwa Serikali imetenga hekta zaidi ya bilioni 3 nchini kwa ajili ya kupanda malisho bora ambayo yatasadia wafugaji kupata chakula cha mifugo yao na hivyo kuondoa migogoro baina ya wafugaji na wakulima.
“Tunataka wafugaji watembelee vituo vya TALIRI ili kujifunza aina za mbegu bora za malisho, namna ya kuzipanda na kuzitunza na hivyo kuweza kuwa na malisho bora kwa mifugo yao sambamba na kujifunza masuala mbalimbali juu ya ufugaji wenye tija, matarajio ya Serikali ni kuona kila mfugaji ana eneo lake la malisho” alisisitiza Mhe. Majaliwa.
Sambamba na hayo Mhe Majaliwa ameitaka TALIRI kuhakikisha kituo hicho ambacho kinathamani ya shilingi bilioni 1.63 ikijumuisha uwekezaji wa vifaa na miundombinu kuhakikisha kinatunzwa ipaswavyo ili Taifa liweze kunufaika kupitia uwezeshwaji huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameeleza kuwa asilimia 67% ya nguvu kazi ya Taifa letu ni vijana, kwa uliona hilo, PASS kwa kushirikiana na TALIRI na kushirikisha Ubalozi wa Denmark mwanzoni mwa mwaka 2018 walikuja na wazo la kuwawezesha vijana kunenepesha mbuzi na hivyo kuanzisha kituo hiki.
Aidha, Mhe. Ulega ameeleza kuwa mradi wa unenepeshaji wa mbuzi ulilenga kuleta mabadiliko chanya kupitia uwezeshaji wa vijana kwa kuwapatia ujuzi wa vitendo juu ya njia bora za unenepeshaji, utafutaji wa masoko, uongezaji wa thamani na kupanua wigo wa vijana kujiajiri. Wapo vijana ambao wameweza kujiajiri na wanaendesha maisha katika sekta ya ufugaji wa mbuzi kibiashara.